Sababu bosi wa zamani Nida, wenzake kukosa dhamana hizi hapa

Muktasari:

Aliyekuwa  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano wamerejeshwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana

Dar es Salaam. Aliyekuwa  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano wamerejeshwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Maimu na wenzake leo Jumanne Januari 29, 2019 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mapya 100, yakiwemo ya kufanya udanganyifu, kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri wao, matumizi mabaya ya madaraka na kutakatisha fedha.

Mbali na Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni meneja biashara wa Nida,  Avelin Momburi; mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers,  Astery Ndege na  ofisa usafirishaji, George Ntalima.

Wengine ni  Xavery Silverius maarufu kama Sliverius Kayombo na mkurugenzi wa sheria, Sabina Raymond.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa Serikali,  Simon Wankyo akisaidia na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leoanard Swai amedai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 7/2019.

Wankyo amedai mbele ya hakimu mkazi, Salum Ally kuwa washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai 19, 2011 na Agosti 2015 katika maeneo mbalimbali  Dar es Salaam.

Imedaiwa kuwa katika kipindi hicho, Maimu, Ndege na Ntalima walikula njama ya  kulaghai Nida kwa lengo la  kujipatia Sh1.175bilioni.

 

Katika shtaka la kuisababishia hasara Nida, Ntalima na Silverius wanadaiwa kati ya Juni 4, 2013 na June 6, 2013 katika Nida washtakiwa waliisababishia hasara mamlaka hiyo kiasi cha Sh 45milioni.

Katika mashtaka hayo, mshtakiwa wa pili( Momburi) na sita(Raymond), wao hawana mashtaka ya utakatishaji.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, hawakutakiwa kusema chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa Mahakama Kuu pekee.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomewa washtakiwa maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo.

Baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 12, 2019.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana kisheria.

Jana Januari  28, 2019 mahakama hiyo iliwafutia kesi  washtakiwa hao baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuieleza mahakama kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.

Washtakiwa hao walifutiwa kesi yao ya zamani, chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai  ( CPA), sura ya 20.