Madai ya rushwa yamfikisha Sabaya kwa RC Kilimanjaro

Muktasari:

Moto wa sakata la Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kudaiwa kulazimisha kupewa rushwa na mmiliki wa Hoteli ya Weruweru River Lodge, Cuthbert Swai unazidi kusambaa kwa kasi

Moshi. Moto wa sakata la Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kudaiwa kulazimisha kupewa rushwa na mmiliki wa Hoteli ya Weruweru River Lodge, Cuthbert Swai unazidi kusambaa kwa kasi.

Safari hii, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amemwita ili kuwasilisha maelezo yake.

Sakata hilo liliibuka Julai 22, katika kikao kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wafanyabiashara wa mkoa huo, kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Naibu Kamishina Mkuu wake, Msafiri Mbipo.

Akizungumza na Mwananchi, Mgwhira alisema alimuita Sabaya ili aeleze upande wake juu ya sakata hilo na baada ya kusikiliza maelezo yake ambayo hakutaka kuyaweka wazi, alisema ameazimia kiitishwe kikao kingine cha wafanyabiashara ili kuwasikiliza.

Mghwira alisema mkoa umeyachukua malalamiko ya mfanyabiashara huyo na kuyafanyia kazi kwa kuwa yalizungumzwa kwenye kikao rasmi.

Alisema malalamiko ya aina hiyo si mara ya kwanza kutolewa na kwamba mkoa umeazimia kukutana na wafanyabiashara kwa ajili ya kusikiliza kero zao na ikibidi utashirikisha wadau wengine.

“Jana (Juzi) tulikaa kwa ajili ya masuala mengine ya kufanyia kazi lakini tukajadili na hilo pia ambalo liko mezani kwetu tunalishughulikia. Tulikubaliana mimi niongee na mkuu wa wilaya kwa sababu yule tayari alishalalamika upande wake halafu tutaitisha kikao cha pamoja na wafanyabiashara na sisi tuwasikilize.”

 

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Jumamosi Julai 27, 2019 kwa taarifa zaidi