Safari miezi mitatu ya hekaheka za Bunge la Bajeti kuanza kesho

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa alisema kiwango kikubwa cha fedha ya bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19, kilienda kwenye miradi ya maendeleo.

Dodoma. Mkutano wa 15 wa Bunge ambao utajikita katika kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2019/20, utaanza kesho.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na bajeti ya Serikali ya mwaka 2019/20 unatarajiwa kukusanya na kutumia Sh33.1 trilioni.

Bajeti hii inayoanza kujadiliwa kesho ni ya pili kutoka mwisho kabla ya kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwaka 2020.

Hiyo inatarajiwa kulifanya Bunge hilo kuwa gumu kwani wabunge wengi watataka kuhakikisha ahadi zao zinakuwapo katika mipango ya Serikali kwani watakuwa wanaingia kwenye ‘lala salama’ kabla ya kwenda kuomba tena ridhaa kwa wananchi.

Hata hivyo, wabunge wa CCM waliohojiwa kuhusu matarajio yao walisema kinachofanyika katika bajeti ya mwaka 2019/2020 ni kukamilisha ahadi walizozitoa katika Ilani za Uchaguzi na zile za Rais Magufuli.

Mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia alisema kwa mtazamo wake, bajeti hiyo ya 2019/20 ndiyo inayokwenda kumalizia ahadi zote zilizotolewa na Rais na zile za ilani ya CCM.

“Ni bajeti ambayo itakwenda kukamilisha utekelezaji wa Ilani ya chama. Maeneo makubwa kabisa ni maji vijijini. Kama unavyojua, tuna tatizo kubwa la maji vijijini na inaenda kutatua tatizo la umeme vijijini,” alisema Mtulia.

Alisema bajeti hiyo itakwenda kushughulikia pia ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu na mradi mkubwa wa kufua umeme wa Rufiji na Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa alisema kiwango kikubwa cha fedha ya bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19, kilienda kwenye miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji (CCM), alisema baadhi ya fedha zilizotegemewa kutoka nje ya nchi hazikuingia lakini za ndani zimetekeleza miradi ya maendeleo hususan inayosimamiwa na kamati yake.

“Ukiangalia miradi iliyo chini ya mahakama imetekelezwa kwa asilimia 75 hadi 80 kwa fedha za ndani. Lakini miradi mbalimbali pia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, imetekelezwa,” alisema Mchengerwa.

Alisema hakuna tofauti kubwa kati ya bajeti ya mwaka 2018/19 na ya 2019/20 na kwamba, fedha zilizotolewa nyingi zilikuwa ni za miradi ya maendeleo.

“Serikali imejitahidi kutoa fedha za ndani na kwa asilimia kubwa zimetoka kama zilivyoahidiwa. Lakini katika bajeti hii (2019/20) kuna maeneo ambayo fedha imeongezeka. Kwa mfano, kwenye Tume ya Haki za Binadamu na Mwendesha Mashtaka Mkuu (DPP),” alisema.

Alisema bajeti hiyo inadhamira kwenda kutibu kiu katika maeneo mbalimbali ya sekta za afya, elimu, maji, miundombinu na kilimo, viwanda, haki za binadamu na demokrasia.

Hata hivyo, wabunge wa upinzani walikosoa vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano wakisema imejikita katika uchumi mkubwa badala ya mdogo ambao unawezesha kuwapo kwa mzunguko wa fedha.

Naibu waziri kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde, alisema fedha za maendeleo zilizotengwa na Serikali kwa bajeti ya 2018/19, ni kidogo.

Mbunge huyo wa Mbozi (Chadema), alisema Serikali imeelekeza fedha nyingi kwenye matumizi ya kawaida kuliko miradi ya maendeleo na kwamba, katika matumizi ya kawaida, asilimia 60 ya lengo ambalo walipanga limetekelezwa.

Alisema sababu nyingine ambayo imefanya miradi mingi kutotekelezwa ni Serikali kujikita kwenye mambo matatu ambayo awali hayakuwepo.

“Mambo hayo ni pamoja na ujenzi wa reli ambao unachukua fedha nyingi za ndani na ununuzi wa ndege,” alisema Silinde.

Alisema kwa kifupi bajeti ya 2019/20 ndiyo ya mwisho kwa kipindi cha kwanza cha awamu ya tano na bajeti inayofuata itakwenda hadi 2020/21.

Mambo ya kukumbukwa

Baadhi ya mambo ambayo yamebaki katika kumbukumbu za Bunge la Bajeti la 2018/19 ni pamoja na wabunge watatu kumwaga machozi bungeni wakitetea hoja zao.

Mbunge wa Welezo (CCM), Dk Saada Mkuya alimwaga machozi alipokuwa akilalamikia ongezeko la bei ya umeme akisema inawaumiza Wazanzibari. Kilio hicho kilisikilizwa na Rais John Magufuli.

Mbunge wa Viti Maalumu CCM), Jacqueline Ngonyani alilia akitaka kulipwa kwa fedha za pembejeo za mawakala zinazotolewa na Serikali.

Katani Ahmed (Tandahimba-CUF) aliililia Serikali akitaka ilipe fedha za ushuru wa korosho uliokuwa unatokana na mauzo nje ya nchi.