Sakata la Sh1.5 trilioni latua kamati ya PAC

Muktasari:

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) jana ilikutana na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mjini Dodoma 

Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeanza kulifanyia kazi sakata la Sh1.5 trilioni.

Hatua hiyo imekuja baada ya kamati hiyo kukutana na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mjini Dodoma jana, huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akilieleza Mwananchi kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo atatoa taarifa ya mwaka ya kamati yake katika mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza wiki ijayo.

Alipoulizwa kama PAC walipokutana na CAG walijadili sakata la Sh1.5 trilioni, Ndugai alisema: “Nina hakika, nina hakika, ila kama nilivyosema mwenyekiti wa kamati atakuja kulieleza hilo huko mbele na mengine wakati wa kutoa taarifa.”

Sakata la fedha hizo liliibuliwa na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alipokuwa akichambua ripoti ya CAG ya 2016/17 alipozungumza na waandishi wa habari Aprili, mwaka jana.

Sakata hilo ambalo tangu lilipoibuliwa na mbunge huyo na kuibukia bungeni katika mikutano ya Bunge, Serikali imeendelea kusema italitolea ufafanuzi katika kamati ya PAC.

Suala la fedha hizo ambazo Zitto alidai hazionekani jinsi zilivyotumika katika ripoti ya CAG, lilipata ufafanuzi Aprili 20, mwaka jana wakati Rais John Magufuli akiwaapisha majaji wapya Ikulu jijini Dodoma.

Rais Magufuli alisema hakuna fedha iliyoliwa na kama ingekuwa hivyo, basi watendaji waliohusika angewachukuliwa hatua.

Akizungumza jana, Ndugai alisema, “(wajumbe wa kamati) wamekutana kweli maana ratiba za PAC zimeanza leo (jana) na zinaendelea kama kawaida maana tulisimamisha nafikiri unakumbuka baada ya hali ya hewa kuharibika tukaona ngoja hali ipite (mzozo kati ya CAG Profesa Mussa Assad na Spika Ndugai).”

“Suala la kujadili haliwezi kusemwa kwa sababu ni mchakato kwa sababu leo (jana) alikuwa CAG na watu wake, kesho (leo) wanakutana na waliokaguliwa na CAG nao watazungumza mambo yao, sasa ukilibeba la CAG inakuwa si nzuri.”

Alisema mkutano wa Bunge ukianza kuna siku kamati ya PAC itapewa nafasi ya kutoa taarifa yake ya mwaka.

Spika alisema, “Hatujapanga tarehe, lakini ni katika Bunge hili na katika taarifa yao watatoa ripoti kueleza mambo yao.”

Wakati akiibua sakata hilo, Zitto alitumia ripoti ya CAG inayoishia Juni 30, 2017 kutoka ukurasa wa 34 unaoonyesha kuwa kati ya Sh25,307.48 bilioni zilizokusanywa, Sh23,792.30 bilioni zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na fedha kwa ajili ya kulipa madeni yatokanayo na amana za Serikali pamoja na riba.

Hata hivyo, Rais Magufuli alipozungumzia suala hilo, alisema, “Kuna ugonjwa tumeupata Tanzania wa kufikiri kila kinachoandikwa kwenye mitandao ni cha kweli. Sifahamu ugonjwa umetoka wapi, lakini ni kwa sababu hii mitandao hatui-control sisi.”

Baada ya kuelezea suala hilo, Rais Magufuli alifikia hatua ya kuwahoji CAG Profesa Assad na katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James kama kuna upotevu wa fedha hizo ambapo wote walikana.