Sasa ni Lowassa vs Chadema

Muktasari:

  • CCM Arusha yasema anatarajia kuungana na wanachama wao wapya 100, Polepole aeleza utaratibu uliotumika kumpokea ikiwamo kuandika barua kwenye tawi lako huko Monduli kuomba kurejea kazi ambayo ameifanya



Dar/Arusha. Sasa ni mpambano kati ya Edward Lowassa na Chadema. Hiyo inatokana na kuwapo kwa taarifa kwamba viongozi na wanachama zaidi ya 100 wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, wanatarajiwa kurejea CCM kumuunga mkono waziri mkuu huyo wa zamani.

Lowassa alirejea CCM hivi karibuni baada ya kutimkia upinzani kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kufuatwa na kundi kubwa la wafuasi wengi kutoka mkoani Arusha.

Alijiunga na Chadema, Julai 28, 2015 ambako alipewa ridhaa ya kugombea urais akiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kabla ya Machi Mosi mwaka huu kurejea CCM akisema “nimerudi nyumbani.”

Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole alisema baada ya Lowassa kuomba kurejea, alielekezwa kuandika barua kwenye tawi lake kazi ambayo alisema aliitekeleza.

“Kesho (leo) ofisi ya CCM Monduli itakuwa na shughuli na vikao, miongoni mwa mambo yatakayofanyika ni kumpokea na kumkabidhi kadi yake ya CCM,” alisema Polepole.

Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe alisema Lowassa atakapowasili saa tatu asubuhi, ataelekea moja kwa moja Monduli ambako atapokewa na viongozi mbalimbali wa CCM wakiongozwa na Polepole ambaye pia ni mlezi wa chama hicho mkoani Arusha.

Kuhusu wanaomuunga mkono Lowassa, Mdoe alisema CCM inatarajia kuwapokea takribani wanachama wapya 100 huku akiwataja baadhi ya viongozi wa Chadema.

Aliowataja ni Onesmo Ole Nangole ambaye kabla ya kuhamia Chadema, alikuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa Arusha. Nangole ambaye ni swahiba mkubwa wa Lowassa, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu suala hilo alisema, “ni kweli kuna hilo jambo, lakini naomba unipe muda kidogo nitakupigia, bado ninatafakari.”

Lakini hadi tunakwenda mtamboni, hakupiga simu.

Baada ya kujivua nyadhifa zote za CCM mwaka 2015, Ole Nangole aligombea ubunge katika Jimbo la Longido kupitia Chadema na kumshinda mgombea wa CCM, Dk Steven Kiruswa.

Hata hivyo, Kiruswa alipinga matokeo hayo Mahakama Kuu ya Arusha na Juni 28, 2016, Jaji Silvangirwa Mwengesi alitengua matokeo hayo na uchaguzi uliporejewa Chadema ilisusia.

Mwingine aliyetajwa na Mdoe ni Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye hata hivyo, alipoulizwa kuhusu hilo alikanusha vikali akisema yupo Dodoma kikazi.

“Nani kasema mimi najiunga na CCM kumufuata Lowassa? Mbona hata kabla ya kuwa upinzani mimi nilikuwa tayari Chadema. Hayo ni maneno tu, mimi nipo Dodoma kikazi,” alisema Lazaro.

Wengine waliotajwa kurudi CCM kumfuata Lowassa ni pamoja na wenyeviti wa vijiji na viongozi wa upinzani kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Arusha.

Awali, ilielezwa kuwa baada ya mapokezi hayo, Lowasaa angehutubia mkutano wa hadhara lakini haikuelezwa ni eneo gani wilayani Monduli.

Kuhusu hilo, Mdoe alisema, “shughuli yote hiyo itafanyika kwenye kikao cha ndani kitakachofanyika eneo la CCM Monduli.