Serikali kuendeleza vita dhidi ya mimba za utotoni

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Mzee Mkongea Ali, kaiweka jiwe la msingi leo, katika jengo la bweni la shule ya sekondari Kasange iliyopo halmshauri ya Kasulu mji. Picha na Happiness Tesha.

Muktasari:

Mbio za mwenge zazindua bweni la wasichana wa Shule ya Sekondari ya Kasange, halmashauri ya mji Kasulu, lengo likiwa ni kuwalinda wanafunzi wa kike dhidi ya mimba za utotoni

Kasulu. Katika kupambana na mimba za utotoni kwa watoto wa kike, Serikali imejenga jengo la bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Kasange iliyopo halmashauri ya Kasulu mji mkoani hapa.

Akizungumza leo, Jumamosi, Aprili 20, 2019, kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Mkongea Ali, wakati wa kuweka jiwe la msingi katika shule hiyo, amesema bweni hilo litasaidia kwa wanafunzi wanaotoka mbali na eneo la shule.

Amesema lengo la Serikali ni kuwasaidia na kuwanusuru watoto wa kike na mimba za utotoni pamoja na kupandisha kiwango cha ufaulu wao.

"Pamoja na Serikali kuweka mikakati yake katika elimu hasa kwa watoto wa kike ni jukumu la wanafunzi hao kuonyesha juhudi katika masomo yao na kuleta matokeo bora.

Kwa upande wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Joyce Ndalichako, amewataka wanafunzi kuacha mara moja kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kwani jambo hilo linaharibu mustakabali wa maisha yao.

"Serikali yenu imeamua kuwekeza katika sekta ya elimu na kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri ili msiwe na visingizio vya kushindwa kufanya vizuri katika masomo yenu," amesema Waziri Ndalichako.

Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa bweni hilo, ofisa elimu sekondari halmashauri ya mji Kasulu, Asia Matitu amesema lengo la mradi huo ni kuongeza kiwango cha ufaulu kwa watoto wa kike.

" Gharama za mradi wa jengo la bweni hilo ni Sh193 milioni na kwamba bweni hilo litakapokamilika litahudumia wanafunzi wa kike 80 wanaotembea umbali wa kilomita tano hadi kufika shuleni hapo," amesema ofisa elimu huyo.