VIDEO: Serikali ya Tanzania yaanika mpango kupambana na mbu waenezao dengue

Muktasari:

Wizara ya Afya nchini Tanzania imeandaa mpango wa Taifa wa kupambana na mbu waenezao ugonjwa wa dengue kwa  kutokomeza mazalia yao katika maeneo ya makazi ya watu

Dar es Salaam. Wizara ya Afya nchini Tanzania imeandaa mpango wa Taifa wa kupambana na mbu waenezao ugonjwa wa dengue kwa  kutokomeza mazalia yao katika maeneo ya makazi ya watu.

Akizungumza leo Jumatano Julai 3, 2019 waziri wa Wizara hiyo, Ummy Mwalimu amesema hilo litasaidia kukabiliana na malaria na mlipuko wa homa ya dengue.

Akizungumza wakati wa upuliziaji viadudu katika kata ya Mchikichini jijini Dar es Salaam, Ummy amesema dengue  imewafanya watendaji wa wizara yake kuwaza upya namna ya kukabiliana na mbu.

“Tumekaa na kuona mpango wa Taifa wa kudhibiti malaria wanapaswa  kufanya kazi kwa mtindo  tofauti, isiwe kugawa chandarua na dawa au vipimo pekee sasa twende kwenye mazingira tuhakikishe tunamaliza mazalia ya mbu,”

Kuhusu hali halisi ya wanaougua dengue, amesema jitihada zimefanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam na wagonjwa wamepungua kwa kiasi kikubwa.

“Habari njema ni kwamba wagonjwa wamepungua, Mei 2019 walikuwa 2,759 lakini Juni wamepungua hadi 790. Niwapongeze kwa juhudi zinazofanyia ila nasisitiza wananchi muwe sehemu ya mapambano haya, kila mmoja ahakikishe anatokomeza mazalia ya mbu,” amesema Ummy.