Serikali ya Tanzania yajitosa soko la pamba

Naibu Waziri wa Kilimo, Omar Mgumba akizungumza bungeni alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema soko la zao la Pamba haliendi vizuri kunatokana na bei ya bidhaa hiyo kushuka katika soko la dunia kutokana na vita ya kibiashara kati ya Marekani na China.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imekiri soko la pamba haliendi vizuri na kwamba  imechukua hatua za kukabiliana na hali hiyo kwa kuwadhamini mikopo ya wanunuzi kwenye mabenki.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Juni 25 2019 na Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

Mgumba amesema ni kweli soko la pamba haliendi vizuri na kwamba msimu umefunguliwa tangu Mei 2, 2019 lakini hadi sasa mwenendo wake si mzuri.

“Sababu kubwa tulishatoa bei elekezi ya Sh1,200 lakini kwa bahati mbaya wakati bei ile inatoka soko la Dunia bei zilianza kushuka hasa kutokana na vita vya kibiashara kati ya China na Marekani,” amesema.

Amesema wakati wanapanga bei hiyo elekezi bei ya pamba katika soko la dunia ilikuwa zaidi dola za Marekani 0.75  lakini sasa ni dola za marekani 0.66 kwa hiyo wanunuzi wameshindwa kuingia sokoni kutokana na benki kukataa kuwapa mikopo.

“Kama Serikali imefanya vikao mbalimbali na kikao cha mwisho kimefanyika siku tatu zilizopita jijini Dar es Salaam na wanunuzi wote na tumekubaliana wataingia sokoni kwa bei ile ile ya Sh1200,”amesema.

Mgumba amesema Serikali imedhamini mikopo yao katika benki na kuwaelekeza wasiuze pamba hiyo hadi Agosti.

Amesema kama watauza pamba hiyo kwa hasara basi Serikali itafidia pengo hilo la hasara lakini bei itaendelea kuwa ni Sh1,200.

Mgumba amesema wabunge wamelalamikia bajeti ndogo ya sekta ya kilimo lakini kumekuwa na ongezeko la Sh50 bilioni kwa mwaka huu.

Pia amesema bajeti ya wizara hiyo ni mtambuka na kuwataka wabunge kutoangalia kiasi cha fedha kinachotengwa katika wizara hiyo tu.