Serikali ya Tanzania yasema maduka ya kubadilisha fedha yatafunguliwa baada ya uhakiki kukamilika

Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa CRDB,Dk Charles Kimei(kulia) akiwa miongoni mwa wanahisa wanaohudhuria semina ya mwaka ya wanahisa kwenye kituo cha mikutano AICC jijini Arusha leo.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewatuliza wamiliki wa maduka ya kubalisha fedha ambayo hivi karibuni yalifungwa kwamba yatafunguliwa baada ya Benki Kuu (BoT) kukamilisha uhakiki.

Arusha. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewatuliza wamiliki wa maduka ya kubalisha fedha ambayo hivi karibuni yalifungwa,  kwamba yatafunguliwa baada ya Benki Kuu (BoT) kukamilisha uhakiki.

Akizungumza leo Ijumaa Mei 18, 2019 jijini Arusha katika ufunguzi wa semina ya wanahisa wa Benki ya CRDB, Majaliwa amesema BoT inakamilisha taratibu za kutolewa vibali kwa baadhi ya maduka hayo.

"Msiwe na mashaka vibali vitatoka hivi karibuni kwa maduka maalum ili kuendelea kutoa huduma lakini pia kuna benki zinatoa huduma nzuri ya kubadilisha fedha ikiwepo benki ya CRDB,” amesema

Awali Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameishauri CRDB kuteua moja ya matawi yake jijini Arusha kufanya kazi hadi usiku ili kutoa huduma ya kubadilisha fedha.

Amesema Arusha ni Jiji la kitalii, ili kuondoa adha  kwa watalii huduma ya kubadilisha fedha zinapaswa kuboreshwa zaidi.

Hivi karibuni BOT ka kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama waliendesha operesheni ya kufunga maduka ya kubadilisha fedha, katika majiji ya Arusha na Dar es salaam na manispaa ya Moshi na  kusababisha adha kwa watu kwa wananchi na wageni.