Serikali ya Tanzania yawajibu Mbowe, Zitto

Muktasari:

Katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) baadhi ya wabunge wamehoji Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwashtaki wafanyabiashara kwa kuwabadilishia makosa yanayohusu kiwango kidogo cha fedha na kuyafanya makosa ya uhujumu uchumi.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema wanaoshtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi wanashtakiwa kutokana na sheria iliyopo si vinginevyo.

Kauli hiyo imetolewa jana Jumatatu Aprili 15, 2019 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Kapteni mstaafu George Mkuchika akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya ofisi hiyo mwaka 2019/20.

Katika hoja hizo, baadhi ya wabunge walihoji Takukuru kuwashtaki wafanyabiashara kwa kuwabadilishia makosa yanayohusu kiwango kidogo cha fedha na kuyafanya makosa ya uhujumu uchumi.

Katika mjadala wa bajeti hiyo,  Zitto Kabwe na Freeman Mbowe  walizungumzia kesi za utakatishaji fedha na uhujumu uchumi zilizoipatia Serikali mabilioni ya fedha.

Zitto, kiongozi wa ACT Wazalendo, alihoji sababu za Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukubaliana na baadhi ya washtakiwa na kukubaliana malipo ya mabilioni, Mbowe (mwenyekiti wa Chadema) akisema kesi hizo zimegeuzwa mkakati mpya wa kukusanya mapato.

Hoja zao zilikuja siku chache baada ya kampuni ya Vodacom kutoa taarifa kuwa imefikia makubaliano na DPP ambayo yanahusisha malipo ya Sh5.2 bilioni ili kumaliza kesi ya uhujumu uchumi dhidi ya wafanyakazi watano waliokuwa mahabusu.

Siku hiyo, mkurugenzi wa mtendaji wa Vodacom, Hisham Hendi na wafanyakazi wengine wanne walikiri makosa na suala lao kuisha.

Katika maelezo yake Mkuchika amesema: “Kwa mujibu wa aya ya 21 jedwali la kwanza la sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 1984 makosa yote yanayoainishwa kwenye sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba hiyo isipokuwa tu kwa kifungu cha 15, ni makosa ya uhujumu uchumi.

“Kuhusu watuhumiwa kushtakiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha ni vyema ikafahamia kuwa kifungu cha 3 cha sheria inayokataza kutakatisha fedha namba 12/2006, kosa la rushwa ni mojawapo ya makosa yanayosababisha mtumishi kushtakiwa kwa kosa la utakatishaji fedha. Wanashtakiwa kwa mujibu wa sheria tuliyonayo.”

Kuhusu hesabu za Takukuru kutokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wakati kila mwaka wanatengewa mabilioni ya fedha, Mkuchika amesema: “Fedha zinazopokelewa kwa ajili ya utendaji wa majukumu ya Takukuru zinajadiliwa na Bunge kupitia fungu namba 30 ambalo hukaguliwa na CAG.”