Serikali ya Tanzania yawakumbusha maofisa ugani kutekeleza wajibu wao

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imewataka maofisa ugani kufanya kazi kwa ubunifu  kuwasaidia wakulima na wafugaji kuleta mapinduzi ya kilimo na ufugaji nchini

Arusha. Serikali ya Tanzania imewataka maofisa ugani kufanya kazi kwa ubunifu  kuwasaidia wakulima na wafugaji katika mapinduzi ya kilimo na ufugaji nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana Jumapili Agosti 4, 2019 na mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira katika ufunguzi wa maonyesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini katika viwanja vya Themi, jijini Arusha.

Amesema maofisa hao wanapaswa kufanya kazi kwa weledi maeneo ya vijijini walipo wakulima, kuyatumia maonyesho hayo kama shamba darasa.

Mwenyekiti wa maandalizi ya Nanenane wa kanda hiyo, Richard Kwitega amesema sekta ya uvuvi inatakiwa kuwekewa msisitizo kutokana na kusuasua huku akizitaka taasisi za elimu kuwaleta wanafunzi katika maonesho hayo kujifunza.

Kaimu mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gabriel Daqqalo amesema ujuzi unaopatikana katika maonyesho hayo, wakulima na wafugaji wanatakiwa kuufanyia kazi kwa maelezo kuwa haina maana kufanyika maadhimisho na elimu kwenda bure.

"Elimu hii mnayofundisha mkaifanyie kazi kwani haina thamani kama mtashindwa kuifanyia kazi na kwa kuona mabadiliko katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi," amesema Daqqalo.