Serikali yaanza kugawa bure mafuta kwa wenye ualbino

Muktasari:

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema watu wenye ualbino wataanza kupatiwa mafuta ya kuzuia miale ya jua bure, kutoka katika hospitali za mkoa na wilaya kote nchini.

Dar es Salaam. Serikali imeziagiza hospitali ngazi ya mkoa na wilaya nchini kuhakikisha wanapoagiza dawa na vifaa tiba kutoka Bohari ya Dawa (MSD), wanaagiza mafuta ya kinga ya ngozi kuzuia miale ya jua ‘sun screen lotion’ kwa ajili ya watu wenye ualbino.

Akizungumza katika chakula cha mchana leo Machi 17 katika utoaji tuzo za ‘I CAN’ zilizoandaliwa Taasisi ya Dk Reginald Mengi kwa watu wenye ulemavu, Samia amesema hiyo ni hatua kwa Serikali kuhakikisha huduma za afya kwa watu wenye ulemavu wakiwemo watu wenye ualbino zinaimarishwa.

Alisema kutokana na kuwepo kwa saratani  ya ngozi inayowakabili watu wenye ualbino nchini, huduma hiyo itaanza kutolewa ili kuwakinga dhidi ya saratani hiyo.

“Serikali imetoa maelekezo kwa hospitali zote za Serikali ngazi ya mkoa na wilaya wanapoagiza vifaa tiba kutoka bohari ya dawa (MSD) wameelekezwa kuagiza mafuta ya kinga ya ngozi ya kuzuia miale ya jua (sun screen lotion) yanayotolewa kwa watu wenye ualbino bila malipo,” amesisitiza.

Amesema pamoja na hayo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutoa huduma ya upimaji wa ngozi, macho na matibabu ya saratani katika hospitali za Serikali za Ocean Road, KCMC Moshi, pamoja na Muhimbili.

Amesema pia inaendelea kufanya uhamasishaji wa watu hao kupima afya zao ili kuepukana na vifo vinavyotokana na saratani ya ngozi.

“Serikali imeunda madawati katika wizara, idara na taasisi za Serikali ili kurahisisha ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika mipango ya Serikali,” amesema Samia Suluhu.