Serikali yafuta umiliki mashamba sita ya Mohammed Enterprises Tanga

Muktasari:

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula jana Jumatatu amefanya ziara wilayani Korogwe na kutangaza uamuzi wa Serikali wa kuyafuta mashamba sita ya kampuni ya Mohammed Enterprises Limited (MeTL)

Dar es Salaam. Kampuni ya Mohammed Enterprises Limited (MeTL) imepata pigo baada ya Serikali kutangaza kufuta umiliki wa mashamba sita yenye ukubwa wa ekari 12, 915. 126 yaliyopo Korogwe jijini Tanga.

Uamuzi huo ulitangazwa jana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula mara baada ya kumaliza kutembelea mashamba ya MeTL, kampuni ambayo inaongozwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo.’

Taarifa kwa umma iliyotolewa na kitengo cha habari cha wizara hiyo imesema mashamba yaliyobatilishwa ni kati ya 14 yanayomilikiwa na kampuni hiyo.

Alisema mashamba yaliyofutwa ni yale yaliyopo eneo la Mombo, Mabogo pamoja na Kwalukonge wilayani Korogwe.

Alisema uamuzi huo unalenga kujenga nidhamu kwa waliopewa rasilimali za Serikali kuzingatia masharti ya uwekezaji.

Naibu waziri huyo alisema uamuzi wa kufuta mashamba hayo umefikiwa baada ya mapendekezo yaliyotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kutokana na kutoendelezwa kwa muda mrefu.

Mabula alisema mapendekezo hayo yaliwasilishwa kwa Rais John Magufuli na Wizara ya Ardhi ilifanya ufuatiliaji katika halmashauri husika kuhusu kutoendelezwa kwake. Alisema baada ya kujiridhisha iliwasilisha maombi hayo kwa Rais na kuridhiwa.

Mabula alisema uamuzi huo wa Rais kuridhia ubatilishaji mashamba sita kati ya 14 yanayomilikiwa na Mohammed Enterprises unalenga kuhakikisha wote waliopewa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wanazingatia masharti na taratibu za uwekezaji.

Naibu waziri huyo alisema mashamba ambayo hayajabatilishwa yamewekewa utaratibu kwa nia ya kuyaboresha kwa kuwa baadhi yake yanahitaji maboresho ili yafanye vizuri.

Aliitaka Halmashauri ya Korogwe kupanga mpango wa matumizi bora ya ardhi katika eneo la mashamba yaliyofutwa na kipaumbele kwa watakaopewa maeneo katika mashamba hayo ni wananchi waliokuwa wakiishi katika mashamba hayo na sehemu itakayobaki atafutwe mwekezaji mwingine kwa kuwa lengo la Serikali ni kuwa na uwekezaji wa viwanda.

Mabula alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella kwa kufanya kazi nzuri ya kufuatilia na kusimamia maagizo mbalimbali tangu Rais Magufuli alipoanza kubatilisha mashamba ambayo hayajaendelezwa katika mkoa wake.

Akizungumza katika ziara hiyo, Shigella aliwataka wananchi wa Korogwe kutovamia maeneo ya mashamba yaliyobatilishwa hadi hapo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe itakapopanga matumizi bora ya ardhi katika mashamba hayo.

Alisema ndani ya wiki hii, ataitisha mkutano na wataalamu wa sekta ya ardhi katika mkoa huo pamoja na wale wa Bodi ya Mkonge kuangalia matumizi ya ardhi iliyobatilishwa kwa wananchi.