Serikali yataja mifumo ya ufuatiliaji Ebola

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema tayari imeweka mifumo ya ufuatiliaji katika mipaka ya nchi, viwanja vya ndege ikiwemo kuwafuatilia madereva wa magari makubwa yanayotoka nje ya nchi wakiwemo wafanyabiashara, ili kuhakikisha ugonjwa wa Ebola hauingii nchini.

Dar es Salaam. Wakati Kericho nchini Kenya tayari kunahisiwa kuwa na mgonjwa wa Ebola, Serikali imesema tayari imeweka mifumo ya ufuatiliaji kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi Leo Juni 17, 2019 Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema katika kuhakikisha wanachukua hatua tahadhari zote zinachukuliwa ikiwemo utayari wa wataalamu wenye mafunzo ya kuhudumia wagonjwa.

Tayari kuna maeneo yametengwa kwa ajili ya kuwahifadhi wagonjwa, mifumo ya kimaabara, ufuatiliaji wa wahisiwa, na mazoezi kwa wataalamu wa afya kwa ajili ya utayari.

"Tayari vifaa maalum vimefungwa viwanja vya ndege na mipakani kuangalia kila anayeingia, wanaoenda Congo hasa madereva tuna utaratibu wa kuwafuatilia wanapoingia nchini na pia wanakwenda maeneo gani, lazima tuhakikishe tunafuatilia mnyororo nzima kwa wafanyabiashara waendelee ila wachukue tahadhari," amesema Dk Ndugulile.

Aidha ameitaka jamii itoe taarifa kwa Mamlaka husika pindi wakimbaini mhisiwa.