Serikali yatoa tamko zito uagizaji sukari

Dar es Salaam. Waziri wa kilimo, Japhet Hasunga ametangaza kusitisha vibali vya uagizaji sukari nje ya nchi kwa wazalishaji wa ndani, badala yake Serikali itatumia kampuni nyingine kuagiza.

Akizungumza jana katika mkutano na wadau wa sekta binafsi na wadau wa kilimo, Hasunga alisema lengo la kufanya hivyo ni kuwataka wazalishaji kuongeza nguvu ya kuzalisha nchini.
Alisema tangu waruhusiwe kuagiza sukari nje ya nchi wenye kampuni za kuzalisha sukari wamebweteka na wanashindwa kuviendeleza viwanda vilivyopo nchini.
“Kumekuwa na shida tangu waruhusiwe kuagiza sukari nje, hizi kampuni zinazozalisha bidhaa hiyo nchini zimeshindwa hata kulima miwa ya kutosha na kuwekeza katika mitambo badala yake nguvu kubwa wameiweka kwenye uagizaji nje pekee.”
“Sukari iliyopo ina uwezo wa kuhudumia walaji nchini mpaka Mei lakini kuanzia Juni Serikali itaagiza tani 25,000 hadi 28,000 ili kusitokee uhaba,” alisema.

“Kama kuna wazalishaji walikua wana mpango wa kuomba vibali wasahau kwa kuwa zoezi hilo limeshafungwa, sasa waendelee na uzalishaji pekee mpaka hapo utaratibu mwingine utakapowekwa.”
“Kama wazalishaji wa sukari nchini wataongeza nguvu katika uzalishaji na mikakati ikawekwa sawa ndani ya miaka mitatu Tanzania haitaagiza sukari nje tena kwa kuwa itakuwa inajitosheleza na kukaribisha wawekezaji kujenga viwanda hivyo,” alisema.
Kufuatia hatua hiyo, mkurugenzi wa huduma kwa Wanachama wa Taasisi Binafsi (TPSF), Louis Accaro ameipongeza Serikali kwa kusitisha vibali hivyo lakini akaomba utoaji wa vibali hivyo kwa kampuni nyingine uwe wa muda mfupi.

Katika hatua nyingine, aliiomba Serikali kuwaweka maofisa ugani nchini chini ya wizara ya kilimo badala ya Tamisemi kwani wanashindwa kufanya majukumu yao ipasavyo ikiwamo kuwasimamia wakulima.

Alisema kuna maofisa ugani 11,000 nchi nzima lakini hawafanyi kazi ipasavyo ya kuzunguka vijijini kuangalia wakulima wanafanya nini na kuwasimamia kwa kuwa wapo chini ya Tamisemi badala ya wizara ya kilimo.
Naye Audax Rukonge, mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa Huru la Wadau wa Sekta ya Kilimo (Ansaf) alisema ni jambo zuri kwa Serikali kusitisha vibali vya kuagiza sukari lakini pia ni muhimu kuangalia na muda watakaotoa ili kusije kutokea tatizo.