Sh1.5bilioni zatengwa kupanga matumizi bora ya ardhi

Muktasari:

Migogoro inayotokana na uvamizi katika misitu inaanza kupatiwa ufumbuzi baada ya Wakala wa Huduma za Misitu kuwezesha vijiji vyote vinavyozunguka misitu kupanga matumizi ya ardhi 

Dar es Salaam. Kiasi cha Sh1.5 bilioni zimetengwa mwaka 2019 kwa ajili ya kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji 100 vinavyozunguka misitu.

Zoezi hilo la upangaji wa matumizi bora ya ardhi litafanyika kwa ushirikiano kati ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC).

Akizungumza leo Alhamisi Januari 31, 2019 ofisa mtendaji mkuu wa TFS,  Profesa  Dos Santos Silayo amesema zoezi hilo linalenga kukabiliana na changamoto ya uvamizi wa misitu.

Amesema upangaji huo utawawezesha pia wananchi wanaoishi kwenye vijiji hivyo kupanga matumizi bora ya ardhi  katika vijiji vyao jambo litakalopunguza uvamizi kwenye misitu.

“Mipango bora itawafanya wananchi wapunguze kilimo cha kuhama hama ambacho kwa kiasi kikubwa huchangia kupunguza maeneo ya misitu,” amesema.

Tayari upangaji huo umeshaanza katika vijiji 11 vilivyopo kwenye baadhi ya wilaya katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Pia,  TFS inatarajia kupandisha hadhi misitu mitano mwaka huu kuwa hifadhi za mazingira asilia ili kulinda baionuai iliyopo katika misitu hiyo.

Mkurugenzi wa NLUPC,  Dk Stephen Nindi amesema upangaji zoezi hilo ni njia bora ya kuondoa migogoro kati ya wananchi na wahifadhi wa misitu.

Amesema mipango hiyo inaenda kuwasaidia wananchi kuangalia namna gani ya kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.