Shahidi adai mwanafunzi alipasuliwa fuvu

Moshi. Daktari bingwa wa patholojia katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Alex Mremi ameiambia Mahakama Kuu kwamba mwanafunzi wa Shule ya Scolastica, Humphrey Makundi alikuwa amepasuka fuvu.

Dk Mremi ambaye ni mmoja wa madaktari walioufanyia uchunguzi mwili wa mwanafunzi huyo, alienda mbali na kuieleza mahakama hiyo mjini hapa kuwa alipata jeraha hilo kabla ya kufikwa na umauti.

Daktari huyo ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi huyo, alisema hayo jana mbele ya Jaji Firmin Matogolo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni mmiliki wa shule hiyo, Edward Shayo, mwalimu wa nidhamu, Labani Nabiswa na mlinzi, Hamis Chacha.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande kutoa ushahidi wake, Dk Mremi alieleza kuwa Novemba 19, 2017, aliletewa mwili ambao ulishaanza kuharibika ili aufanyie uchunguzi wa kitaalamu.

“Mwili ulikuwa na majeraha na tulibaini jeraha kubwa kwenye paji la uso lililovunja fuvu la kichwa. Jeraha hilo tulipolipima lilikuwa na ukubwa wa sentimita sita kwa tano,” alieleza daktari huyo.

“Chanzo cha kifo ni jeraha kubwa lililovunja mfupa. Ni jeraha lililosababisha kifo. Mwili ule ulikuwa ni wa mtoto wa kati ya miaka 15 na 17 kutokana na mwonekano wa meno.

“Yalikuwapo na majeraha mengine ambayo ni michubuko mabegani, mgongoni na mapajani. Tulichukua pia mifupa mbalimbali na nyama kwa ajili ya kufanya DNA (vinasaba).”

Shahidi huyo alieleza kuwa baada ya kukamilisha uchunguzi na kuandika ripoti, walichukua sampuli za damu na mate kutoka kwa wazazi akiwamo baba wa marehemu, Jackson Makundi kwa ajili ya DNA.

Shahidi huyo alienda mbali na kueleza kuwa katika uchunguzi wao walifanya uchunguzi ambao kitaalamu unajulikana kama histopathology na kubaini jeraha alilipata akiwa bado yuko hai.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, jopo la mawakili wa utetezi likiongozwa na Elikunda Kipoko, David Shillatu, Wakisa Sambo na Patrick Paul walimuuliza maswali na sehemu ya maswali hayo ilikuwa kama ifuatavyo:-

Wakili Shillatu: Hebu isaidie mahakama. Unafahamu kipimo cha Carbon 14?

Shahidi: Ndio. Ni kipimo kinachotumika kujua umri wa mhusika

Wakili Shillatu: Umeiambia mahakama mlikadiria umri wa marehemu. Ni kweli au sio kweli?

Shahidi: Ni kweli

Wakili Shillatu: Hebu isaidie mahakama ni kwa nini hamkutumia kipimo cha Carbon 14?

Shahidi: Ziko njia nyingi za kupata majibu. Huwezi kutumia gharama kubwa kupata majibu mepesi.

Wakili Shillatu: Naomba isaidie mahakama kama kipimo cha Carbon 14 kingetumika kingekuwa na majibu sahihi zaidi?

Shahidi: Nakataa hata kama tungetumia Carbon 14 naamini itatupa majibu hayahaya.

Wakili Sambo: Umeeleza jeraha lile lilikuwa ni kabla ya kifo?

Shahidi: Ni kweli

Wakili Sambo: Hebu ionyeshe mahakama hicho ulichosema kipo page (ukurasa) gani katika kielelezo cha mahakama P1?

Shahidi: Report (taarifa) hii iliandikwa mara tu baada ya uchunguzi. Majibu hayo hayapo hapa.

Wakili Sambo: Polisi walivyoleta huo mwili walisema una umri gani?

Shahidi: Kwenye hilo police form (fomu ya polisi) namba 99 ilieleza ni mtu mzima miaka 40 hadi 44

Wakili Kipoko: Hebu nisomee hapa kwenye hii postmoterm report (taarifa ya uchunguzi) umeandika nini?

Shahidi: Mwili ulikuwa una not less than two weeks (sio chini ya wiki mbili) tangu afariki.

Wakili Kipoko: Hebu ukiondoa hizo wiki mbili ni lini kifo kilitokea?

Shahidi: Inaweza kuwa 5 (5.11.2017) au tarehe 4 (4.11.2017) kushuka chini

Wakili Paul: Shahidi, utakubaliana na mimi wiki mbili ni siku 14?

Shahidi: Ni kweli

Wakili Paul: Kwa hiyo mtu aliyefariki tarehe 5 hawezi kuwa hai tarehe 6?

Shahidi: Ndio

Mwanafunzi huyo alitoweka shuleni Novemba 6, 2017, na baadaye kubainika ameuawa na watu wasiojulikana baada ya maiti ya mtu aliyedaiwa ni mtu mzima mwenye ndevu, kufukuliwa kwa amri ya mahakama.

Mwili wake uliokotwa Novemba 10, katika Mto Ghona, mita zipatazo 300 kutoka shuleni hapo.