UCHOKOZI WA EDO : Shangazi Fatma anatuacha vinywa wazi kwa ujasiri wake

Fatma Karume

Muktasari:

  • Labda ni raha ya kuwa mtoto wa Rais mstaafu, labda ni raha ya kuwa mjukuu wa Rais mstaafu. Bibi yake alikuwa ‘first lady’ pale Zanzibar. Mama yake akawa first lady. Inawezekana ana kinga nyingi kando yake lakini naona mioyo ya wengine ingetamani kinga zake.

Anajiita shangazi wa Taifa, Fatma Karume. Wengi tunamwangalia kwa mshangao. Wakati mwingine tunamtazama kwa wivu. Ujasiri wake wa kusema anachojisikia nyakati hizi ni mkubwa. Anaongea kama vile yupo katika nyakati za tawala zilizopita.

Ni mtoto wa Rais mstaafu. Si mwanasiasa wa upinzani. Kitaaluma ni mwanasheria wa kawaida ingawa katika cheo ni Rais wa Wanasheria. Anawezaje kuwa na ‘kiburi’ cha kuongea anavyojisikia? Inaacha midomo wazi. Wengi wanatamani kuwa yeye lakini hawawezi. Sijui wanachohofia lakini ni wazi kwamba kama kipo basi Shangazi Fatma hakioni.

Labda ni raha ya kuwa mtoto wa Rais mstaafu, labda ni raha ya kuwa mjukuu wa Rais mstaafu. Bibi yake alikuwa ‘first lady’ pale Zanzibar. Mama yake akawa first lady. Inawezekana ana kinga nyingi kando yake lakini naona mioyo ya wengine ingetamani kinga zake.

Wametengeneza ushkaji wa katika korido za mahakamani na mwanasiasa Zitto Kabwe. Unaweza kumwelewa Zitto kwa miaka mingi. Ni Mwanasiasa anayejua kujenga hoja. Wakati mwingine anajua kujiwahi mapema kwa maneno kama vile ‘wanataka kuniua’, ‘kuna njama za kunikamata’ au ‘jana wamenifanyia kikao’. Lakini huyu Shangazi yeye hana muda huo. Anaongea kama vile hajadiliwi na upande wa pili.

Nataka kuona mwisho wake katika maongezi yake magumu ya kila siku. Waswahili tulioishia darasa la saba tumebakia na maswali tu. Ataambiwa na baba yake anyamaze au ataendelea hivi hivi? Baba yake ana msimamo gani kuhusu kauli za mwanae? Je baba yake na Namba Moja hawajawahi kuteta kuhusu huyu mtoto?

Inatia shauku kuendelea kumsikiliza huku pia tukiendelea kusubiri upande mwingine unachofikiri kuhusu yeye. Amecharuka sana katika zama hizi. Wakati ule wa zamani tulikuwa na mtoto wa rais mstaafu aliyecharuka. Makongoro Nyerere. Lakini yeye hakuwa kama huyu na hata nyakati alizotamba kama mwanasiasa wa upinzani hazikuwa nyakati kama hizi.

Tuendelee kutazama hii filamu zaidi na zaidi. Itaishia wapi? Huyu Shangazi wa Taifa ataishia wapi? Zamani nilikuwa natafakari kuhusu uzuri wake, siku hizi natafakari kuhusu mdomo wake tu. Namsikiliza natabasamu. Nafsi yangu huwa haijadili kama anachosema ni sahihi au sio sahihi, najadili ujasiri wake.