Siasa, neema zinavyopamba ziara za Waziri Mkuu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na mkazi wa Mndami Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ambaye ni mlemavu wa miguu, Stephine Kwayu wakati akiwaaga wananchi kuelekea Rombo kuendelea na ziara. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

  • Majaliwa, ambaye yupo mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya siku tatu aliyoianza juzi, alisema kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa isimamie sheria zilizowekwa mipakani.

Rombo. Ziara za Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa zinaweza kuwa neema kwa wananchi, na moto kwa viongozi wa mkoa na wilaya baada ya jana kumuweka katika hali ngumu mkurugenzi wa halmashauri.

Majaliwa amempa siku 15 mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kuwalipa wafanyakazi wa madini ya pozolani Sh114 milioni wanazodai, jambo ambalo ni neema kwa wananchi hao.

Na hayo ni baadhi ya matukio yanayotawala ziara zake mikoani. Waziri Mkuu ametokea mikoa ya Kigoma na Kagera, ambako pia alikemea na kuonya dhidi ya vitendo visivyofaa vya viongozi.

Lakini pia anawataka viongozi kuanza maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuzungumza mazuri yanayofanywa na CCM.

Mbali na kumpa siku hizo 15 mkurugenzi huyo, Waziri Mkuu alitaka uongozi wa mkoa kuwa makini na mpaka wa Holili, ambao alisema si salama na kwamba unaweza kusababisha watu wabaya kama wanaofanya mauaji ya Njombe kujiingiza nchini kirahisi.

Jana alionyesha ukali kwa mkurugenzi huyo, Magreth John alipojaribu kueleza kuwa madai halisi ya wafanyakazi hao ni Sh12 milioni na si kama walivyoandika kwenye mabango yao waliyonyoosha juu wakati wa kumpokea.

“Mkurugenzi usibishane na mimi, wananchi hawa wanadai zaidi ya Sh100 milioni na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) inaonyesha wanadai kiasi hicho cha fedha,” alisema Waziri Mkuu.

“Mkuu wa Mkoa naomba ulisimamie jambo hili la kuhakikisha wananchi wanalipwa fedha zao zote na ukija Dodoma nipate hii taarifa ya malipo yao.”

Mkuu huyo wa mkoa, Anna Mghwira aliungana na Majaliwa kueleza kuwa fedha ambazo wanadai ni Sh114milioni.

Kuhusu mpaka wa Holili, Waziri Mkuu alisema kuna viashiria vya uvunjifu wa amani, baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na wananchi.

Majaliwa, ambaye yupo mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya siku tatu aliyoianza juzi, alisema kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa isimamie sheria zilizowekwa mipakani.

Alibainisha kuwa baadhi ya watu hawana nia njema wanaingia mipakani kutokana na matukio yanayoendelea huku akitoa mfano wa mkoani Songwe.

“Mpaka wetu huu una matatizo makubwa, ili tuimarishe usalama kwa nchi zote mbili ni lazima sheria zilizowekwa kwa nchi zote mbili zizingatiwe. Ni lazima tulinde mipaka yetu ili tubaini wanaoingia tuwajue na tujiridhishe ili haya mambo yanayoendelea mipakani yakome,” alisema Majaliwa.

Akiwa mkoani Kagera na Kigoma hivi karibuni, kiongozi huyo alitambulishwa kama mlezi mpya wa CCM wa mikoa hiyo.

Baada ya kupokelewa eneo la Nyakanazi Wilayani Biharamulo,Waziri Mkuu Majaliwa alimwaga ahadi nyingi za kuboresha maisha ya wananchi na kusifia kazi kubwa ambayo tayari imefanywa na Serikali.

Lakini akaonyesha kutoridhishwa na ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hiyo na pia kukerwa na mvutano kati ya mkuu wa wilaya hiyo, Saada Malunde na mkurugenzi wa halmashauri, Wende Ng’abala

Alisema mgogoro huo unahusisha ‘kushikana uchawi’, akisema ni kitu cha aibu na kuwataka wajipime kama bado wana sifa za kuendelea kuwa watumishi wa umma.

Waziri Mkuu aliahidi kupeleka fedha za kujenga kituo cha maegesho ya magari ambayo huelekea nchi jirani za Rwanda na Burundi.

Hali ilikuwa kama hiyo mjini Bukoba, ambako alianzia kwenye jengo la kitega uchumi cha CCM kilichotelekezwa kwa zaidi ya miaka ishirini.

Alisema siri ya CCM imejificha kwenye uwekezaji wa majengo na umiliki wa viwanja vya michezo na kuwataka viongozi kuanza maandalizi ya kunadi mazuri yaliyofanywa na chama hicho.

Kuhusu zao la kahawa, Waziri Mkuu alizitaka mamlaka kuanza maandalizi mapema ili kuepuka lawama zilizoonekana msimu uliopita na kutaka mfumo wote za zao hilo uangaliwe upya kuanzia kwa mkulima hadi kwenye masoko.

Lakini akageukia siasa akisema Serikali imejikita kwenye maeneo muhimu yanayogusa wananchi moja kwa moja na kuwa ni wajibu wa viongozi kufuatilia utekelezaji wa ilani ya CCM.

“Leo tuna miaka mitatu,chama lazima kijiridhishe angalau tuna nusu ya kura tunazozihitaji au zaidi,” alisema Majaliwa.

Kama ilivyokuwa katika mikoa mingine, Majaliwa aliwageukia wakurugenzi wa halmashauri za wilaya hiyo, akiwataka kuacha malumbano na kutoa taarifa kwenye vikao vya chama na kuwataka kujipanga kwa uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.

Nyongeza na Phinias Bashaya na Happiness Tesha