Siri ya Kenya kuwadhibiti magaidi katika shambulio la Hoteli ya DusitD2

Monday January 21 2019

 

Nairobi, Kenya. Kenya ni moja ya nchi za Afrika zinazoandamwa na matukio ya kigaidi na katika miaka ya karibuni takribani matukio manne makubwa yamefanyika na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Miongoni mwa matukio makubwa yaliyoingia katika historia ya Kenya ni lililohusisha kushambuliwa kwa ubalozi wa Marekani jijini Nairobi, Agosti, 1998 ambapo watu 213 waliuawa.

Tukio hilo lililohusishwa na mtandao wa kikundi cha Al Qaeda chini ya aliyekuwa kiongozi wake, Osama bin Laden, lilitokea wakati mmoja na lile lililoukumba ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam ambako watu 11 waliuawa na wengine 85 kujeruhiwa.

Tukio lililofuata ni lile lililohusisha mashambulizi mawili yaliyofanyika kwa wakati mmoja mwaka 2002, moja likiilenga ndege ya Israel katika Uwanja wa Ndege wa mjini Mombasa huku lingine likitupwa katika hoteli ya kitalii ya Kikambala muda mfupi baada ya watalii 60 kutoka Israel kukamilisha usajili wa kukaa hotelini hapo. Watu 13 waliuawa 10 wakiwa ni Wakenya.

Mwaka 2013 Al Shabaab walivamia jengo la Westgate lililokuwa na mkusanyiko wa huduma mbalimbali yakiwamo maduka makubwa na kuua watu 67. Mwaka mmoja baadaye kikundi hicho kilijinasibu kufanya mashambulizi katika eneo la Mpeketoni, Kaunti ya Lamu kati ya Juni 15 na 17, 2014 ambako watu 60 waliuawa.

Hata hivyo, katika mashambulizi yote hayo vikosi vya Kenya vilikuwa vikichukua muda mrefu kukabiliana na magaidi hadi kuzima mashambulizi na hivyo kusababisha idadi ya waliokufa kuwa kubwa na kushuhudiwa wengine wengi wakipata majeraha na hata uharibifu wa mali kuwa mkubwa zaidi. Hali imekuwa tofauti katika tukio la kushambuliwa kwa hoteli ya DusitD2 lililotokea wiki iliyopita ambapo watu 14 walithibitika kupoteza maisha huku magaidi wote watano waliotekeleza shambulizi hilo nao wakiuawa.

Ilichukua takriban saa moja tu kuanza kwa harakati za kuokoa raia, kuwadhibiti magaidi na kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo la Riverside ilipo hoteli hiyo na mengineyo.

Ndani ya muda mfupi baada ya kutokea kwa shambulizi la DusitD2 vikosi vya ulinzi viliwasili, watoa huduma za dharura za kitatibu yakiwemo magari ya kubebea wagonjwa yaliwasili, kituo cha kutolea habari kiliandaliwa na kubwa zaidi kuimarika kwa mshikamano miongoni mwa viongozi wa kisiasa bila kujali tofauti zao.

Kikosi maalumu

Ufanisi wa kikosi maalumu kilichopewa jukumu la kupambana, kuzima na kufanya uokozi katika matukio makubwa

yakiwamo ya ugaidi ni miongoni mwa mambo yaliyofanikisha kuwakabili magaidi katika shambulio hilo.

Kikosi hicho cha Kenya maarufu kama Recce Squad, kilichopata mafunzo ya hali ya juu nchini Israel na Marekani, kilifika eneo la hoteli hiyo na kuanza uokoaji na mapambano dhidi ya magaidi hao mapema kuliko ilivyokuwa katika matukio mengine ya kigaidi yaliyowahi kuikumba Kenya.

Recce ambao idadi kamili ya askari wake, silaha wala nguvu yake haifahamiki vizuri inafanishwa na vikosi maalumu kama SAS cha Uingereza, Delta Force (Marekani) EPIGN (Ufaransa) na Sayaret Matkal cha Israel.

Kenya imepokea pongezi nyingi kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Marekani kwa jinsi ilivyoweza kukabiliana na shambulio hilo, kuokoa raia na kuwamaliza magaidi waliohusika.

Askari wa Uingerza alivyosaidia uokoaji

Miongoni mwa picha zilizosambaa na kutazamwa zaidi kuhusiana na tukio hilo ni ile ya askari wa kikosi cha SAS cha Uingereza ambaye ilielezwa kwamba alifika eneo hilo kusaidia uokozi na mapambano dhidi ya waliohusika na shambulio hilo.

Askari huyo ambaye hakutajwa jina, alionekana akiwa amejiimarisha kwa silaha mbalimbali ikiwamo bunduki ya kivita mikononi huku akiwa amevaa vazi maalumu lililobeba silaha nyingi kama bastola, kisu, mabomu na risasi huku kichwani akiwa amejifunga kitambaa kilichofunika kichwa chote na kubakiza sehemu ya macho tu.

Mpambanaji huyo anayeelezwa alikuwa Kenya kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vikosi vya nchi hiyo, amewahi kushiriki katika vita mbalimbali ikiwamo ya nchini Syria dhidi ya wapiganaji wa Dola ya Kiislamu (ISIS).

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kenya, wakati shambulio hilo likitokea askari huyo alikuwa mjini humo kwa ajili kupata mahitaji mbalimbali dukani na kwamba alipobaini kuna tukio la kigaidi alijiandaa ndani ya muda mfupi na kuingia kazini na kufanikiwa kuokoa raia wengi.

Mtu huyo ambaye wengi waliookolewa walimwelezea kuwa ni jasiri na shupavu, inaelezwa kwamba anatarajiwa kupewa tuzo ya medali ya ushujaa ya George Cross kutambua kazi kubwa aliyoifanya kuokoa watu waliokuwa katika hatari ya kuuawa. Medali hiyo ni ya pili kwa ukubwa kati ya medali za ushujaa zinazotolewa nchini Uingereza ikitanguliwa na ile ya Victoria Cross.

Taarifa zinaeleza kwamba askari huyo alikuwa katika kikosi maalumu cha SAS kilichokuwa kikipambana na ISIS nchini Syria na kufanya kazi kwa mafanikio makubwa.

SAS imegawanyika katika matawi manne ya A, B, D na G huku kila moja likiwa limekamilika katika idara zote kwa kuwa na wataalamu wa kijeshi wa anga, majini na ardhini.

SAS ni kikosi maalumu cha Kijeshi cha Uingereza kilichoanzishwa mwaka 1941 kwa ajili ya kutekeleza majukumu mazito ikiwamo kukabiliana na magaidi, kuokoa mateka na mapambano. Taarifa za kikosi hicho ni siri kubwa ambayo haitolewi hadharani.

Jinsi magaidi walivyoingia

Mkanda wa video uliochukuliwa kutoka katika kamera za usalama (CCTV) na kuonyeshwa kupitia vyombo vya habari vya Kenya hususan Citizen TV, unaonyesha jinsi magaidi hao walivyoingia hotelini hapo wakipitia eneo la mgahawa na mmoja wao kujilipua alipofika mgahawani hapo.

Watano wapandishwa kizimbani

Watu watano akiwamo raia wa Canada, wamepandishwa kizimbani wakihusishwa kwa kuwasaidia waliotekeleza tukio hilo.

Watu hao ambao wanne kati yao ni wanaume na mwanamke mmoja, walifikishwa kizimbani Ijumaa iliyopita wakiwa ni sehemu ya watu 11 wanaodhaniwa kuhusika na tukio hilo.

Guleid Abdihakim mwenye uraia wa Canada anasadikiwa kufanya mawasiliano na wahusika hao huku Gladys Kaari Justus akichunguzwa kwa kuwasaidia watu hao kuhamisha fedha.

Joel Ng’ang’a Wainaina na Oliver Kanyango Muthee ambao ni madereva taksi wanatuhumiwa kwa kuwasafirisha waliotekeleza tukio hilo mpaka mahala hapo na mtuhumiwa Osman Ibrahim anachunguzwa akiaminika kukutana na mmoja wa magaidi hao, Januari 8, mwaka huu.

Imeandaliwa na Suleiman Jongo kwa msaada wa mitandao mbalimbali. Maelezo ya ndani, Aurea Simtowe.


Advertisement