Sirro akerwa uhalifu ujenzi reli ya kisasa

Mkuu wa Polisi nchini (IGP) Simon Sirro

Muktasari:

  • Kuhusu uhalifu, Sirro alitoa onyo kwa wanaojihusha nao hasa wizi wa mafuta huku akiagiza uongozi wa kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga reli hiyo kuwa na kumbukumbu za picha na kupata taarifa za walinzi wa jadi wa jamii ya Kimasai wanaolinda mali za mradi huo ili kuondoa usumbufu.

Morogoro. Mkuu wa Polisi nchini (IGP) Simon Sirro ameahidi kujenga vituo vya polisi maeneo yanayopitiwa na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge), ili kuimarisha ulinzi.

Kamanda Sirro alisema hayo jana mkoani Morogoro alipokagua ujenzi wa reli hiyo, alianzia eneo la Ngerengere wilayani Morogoro mpaka Kilosa.

Pia, Sirro alieleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi na kuahidi polisi itazidi kuimarisha ulinzi eneo la mradi hadi utakapokamilika. “Kasi inayoendelea katika ujenzi huu naridhishwa nayo kwani juhudi zinaonekana, kutokana na umuhimu wa mradi huu nimedhamiria kuongeza ulinzi wa kutosha maeneo yote ya mradi,” alisema.

Alisema kumekuwa na taarifa mbalimbali za uhalifu kwenye mradi huo hususan miundombinu na kwamba baada ya kukamilika vitajengwa vituo vya polisi. Hata hivyo, hakutaja idadi.

“Huu mradi ni mkubwa lakini kuna watu wanafanya hujuma ya mali za umma zinazotumika kujenga reli yenye nia njema kwa taifa, watakaohusika watashughulikiwa kisheria,” alisema.

Kuhusu uhalifu, Sirro alitoa onyo kwa wanaojihusha nao hasa wizi wa mafuta huku akiagiza uongozi wa kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga reli hiyo kuwa na kumbukumbu za picha na kupata taarifa za walinzi wa jadi wa jamii ya Kimasai wanaolinda mali za mradi huo ili kuondoa usumbufu.

Awali, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa, alisema mradi huo unaendelea vyema na utakamilika kwa muda uliopangwa.

Pia, alimshukuru Sirro kwa kuwatembelea na kuahidi kujenga vituo vya polisi.

Ujenzi wa reli hiyo itakayotumia umeme unaanzia jijini Dar es Saalam mpaka Morogoro kwa gharama ya Sh2.8 trilioni kwa fedha za Tanzania, inaendelea kujengwa kwa kiwango cha kisasa na kimataifa na treni itakuwa na spidi ya kilomita 160 kwa saa.