Spika azungumzia kutimua wabunge, adai ni wakorofi

Dodoma. Spika wa Bunge Job Ndugai amesema amekuwa akitimua wabunge vikaoni kwa kuwa ni wakorofi na kuahidi kuendelea kufanya hivyo baada ya Bunge la Bajeti lililomalizika Juni 28 kutawaliwa na adhabu hizo.

Ndugai, ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mkoka wilayani Kongwa, pia alitumia nafasi hiyo kuwapigia kampeni wanachama watakaoteuliwa na CCM kugombea uongozi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu, akisema wasimuangushe Rais John Magufuli.

Katika Bunge la Bajeti lililoanza Aprili 2, wabunge wawili wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Godbless Lema (Arusha Mjini) walipewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge baada ya kuunga mkono kauli kwamba chombo hicho ni “dhaifu”.

Mdee amefungiwa kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge baada ya kuunga mkono kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad aliyetumia neno “udhaifu wa Bunge” wakati alipoulizwa sababu za mapendekezo yake kutofanyiwa kazi.

Wakati Bunge likijadili mapendekezo ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu kauli ya CAG, Lema alirudia maneno hayo kuwa “Bunge ni dhaifu”, kauli iliyomfanya Naibu Spika Dk Tulia Ackson kumshtaki kwa kamati hiyo na hivyo kufungiwa mikutano mitatu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mkoka kilichopo wilayani Kongwa, Ndugai alisema Bunge la Bajeti lilikuwa na mambo mengi.

“Mengine nayaamua mwenyewe, mengine Bunge linaamua wengine wakorofi korofi nafukuza,” alisema Ndugai ambaye katika Bunge lililopita pia alimuandikia mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) kumueleza kuwa kiti cha ubunge cha Singida Mashariki, kilichokuwa kikishikiliwa na Tundu Lissu, kiko wazi kwa kuwa haonekani bungeni wala hospitalini.

“Ikishakuwa ni ukweli na haki na wewe ni kiongozi, lazima usimame kwenye ukweli, haki na sheria, Katiba na miongozo mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa baadhi ya watu ni jeuri na wameamua kujitenga na kusimama kwenye ujeuri. “Sasa inakuaje si inabidi hatua zichukuliwe? Kwa hiyo hayo hayo ya huko nyie yaacheni huko,” alisema.

Akichanganya na lugha ya kigogo katika hotuba yake, Ndugai alisema wakati akiwania ubunge 2015, watu walisema ni mkali anapiga watu kwa fimbo.

Alikuwa akirejea tukio lake la kumchapa na bakora mgombea mwenzake wa ubunge ndani ya CCM wakati wa mkutano wa kujinadi.

Alisema hivi karibuni mtu huyo alimpigia simu na kumtania kwa kumuuliza kama bado anatembea na fimbo na yeye akamjibu kuwa siku hizi ameacha.

Alisema walifurahi kwa pamoja na wanafanya kazi pamoja.

“Kwa hiyo hayo katika magazeti muwe mnasoma Ndugai kafanya hivi kafanya hivi msiwe mnayajali sana,” alisema.

“Siasa ndivyo zilivyo. Ila ninapoamua huwa simuonei mtu naangalia haki na ukweli uliko.”

Uchaguzi serikali za mitaa

Ndugai aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kuchagua wagombea wa CCM na wagombea wanaoteuliwa na chama hicho wawe wazuri.

“Hatutaki madoamadoa. Kiongozi awe mzuri lakini wa CCM. Kama mna kiongozi mzuri lakini hajajiandikisha, kamuandikisheni msije mkatuambia hana kadi. Hakuna hii biashara nyingine, haitusaidii, hatuwezi kusogea,” alisema.

“Kwani kule bungeni mie si ndio mkubwa wao. Nawaambia hawafai hao sasa hamnielewi nini mimi. Kwani hao wakina (mwenyekiti wa Chadema, Freeman) Mbowe, mkubwa wao ni nani?”

Alisema sababu zake ni kwamba uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unaendana na uchaguzi mkuu isipokuwa mmoja unatangulia. “Uchaguzi wa mwakani tunataka sisi wa Dodoma tumpe Dk John Magufuli kura za kutakata. Huyu ni Rais wa mfano,” alisema.

“Huwezi uchaguzi huu (wa serikali za mitaa) umemwekea mabakamabaka halafu mwakani unamchagua ili iweje sasa? Kama kura yako mbaya iwe mbaya tu mwaka huu na mwakani.”

Alisema wakazi wa Dodoma wakiacha kumchagua Rais Magufuli mwakani watakuwa wamefanya dhambi kubwa kutokana utekelezaji wa nia ya kuhamishia makao makuu Dodoma.

Vijana hawafanyi kazi

Ndugai aliwashauri vijana wa jimbo lake kujishughulisha na shughuli za uchumi ili wajiajiri na kuinua vipato vyao na kuacha kucheza pool kwani ni ujinga.

“Wakina mama kazi yenu kuwapikia ugali na kuwatengea. Tuwaache mtufundishie kufanya kazi. Mtoto wako wa sekondari afanye kazi. Ajifunze kununua kalamu na shati mwenyewe,” alisema.

Aliwataka vijana kuacha kuchagua kazi na kufanya biashara yoyote inayowatengenezea fedha bila kuona aibu.

Naye mbunge wa viti maalum (CCM), Mariam Ditopile alisema vijana Dodoma wana changamoto ya kazi na wakipewa mikopo wanageuza nauli za kuendea Tanga.

“Nimezunguka mkoa huu nimeona heshima kubwa tuliyopewa na Rais Magufuli. Alianzisha elimu bure mnufaika hapo ni kijana. Hapohapo akaanzisha operesheni ya hakuna mwanafunzi kukaa chini,” alisema.

Alisema kwenye uchaguzi mkuu wa 2015 walifanya tathimini na kubaini vijana walikuwa wakisumbua kutokana na dawa ya kulevya na pombe kali za viroba.

“Unaona watu wanakuzungushia mikono (ishara ya kutaka mabadiliko iliyokuwa ikitumiwa na wapinzani 2015), kumbe tayari kashawaka huyo,” alisema.

“Sasa hivi mnaingia 2020 (uchaguzi mkuu) vichwa vyeupe tuone kama mtapewa Sh5,000 kwa ajili ya kuwarusha akili zenu muache kufuata yale mnayoambiwa na wazazi wenu,” alisema.

Awali Ndugai alifungua kisima katika Shule ya Msingi Mkoka inayojumuisha watoto wenye ulemavu. Kisima hicho kilijengwa na Mariam Ditopile.