Steve Nyerere adai kufuatiliwa na ‘wasiojulikana’

Tuesday November 13 2018

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Mchekeshaji, Steve Nyerere amesema kuna watu wasiojulikana wamekuwa wakimfutilia kwa siku tatu mfululizo hali inayotishia usalama wake.

Akizungumza na MCL Digital, Steve aliyejipatia umaarufu kwa kuigiza sauti za viongozi mbalimbali nchini amesema aliligundua hilo juzi baada ya kutaarifiwa na mlinzi wake wa nyumbani.

Amesema mlinzi wake ndiye aliyekuwa wa kwanza kugundua kufuatiliwa kwake na alipochunguza alibaini kuwa yupo hatarini.

“Mlinzi aliniambia kuwa ameona gari likisimama nje ya nyumba yangu kwa siku mbili, yaani ni kama vile limekuwa likinifuata kwa nyuma na ninapoingia ndani hubaki nje kwa dakika kadhaa kisha huondoka,” amesema.

Alisema alipopata taarifa hizo alifuatilia na kweli juzi aliona gari likimfuatilia mpaka getini kwake na alipoingia ndani liliondoka.

“Kwa kweli nimetishika sana kwa sababu sijui nafuatiliwa kwa sababu gani, nimetoa taarifa hizi sehemu husika na nina imani hakuna jambo baya litanipata,” amesema.

 


Advertisement