Sugu apiga ‘show’ kwa wapiga kura wake

Saturday December 1 2018

 

By Godfrey Kahango, Mwananchi [email protected]

Mbeya. Baada ya miaka sita kutopanda jukwaani kuwaburudisha wakazi wa Jiji la Mbeya, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ jana usiku Ijumaa Novemba 30, 2018 aliutumia vyema kwa kuwaburudisha vya kutosha wakazi wa Jiji  hilo.

Sugu alitoa burudani hiyo katika ukumbi Green Lounge, uliopo Mbeya City Pub-Mwanjelwa na huku akielezea dhumuni kuu la ‘show’ yake hiyo ni  baada ya kutopanda jukwaani kwa takribani miaka sita kwa wananchi wa Jiji hilo.

Kwa mara ya kwanza Sugu akiwa Mbunge mwaka 2012 alifanya ‘Show’ katika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya na kuwaalika wasanii wengine na fedha zote zilizopatikana alinunua mahindi ambayo aliwapelekea kama msaada waathirika wa mafuriko yaliyotokana na mvua katika mtaa wa Iyunga Jijini hapa.

Sugu alitumia takribani saa moja na takika 25 kutumbuiza bila kupumzika huku mashabiki waliofurika ukumbini hapo walionekana kucheza naye bila kuchoka mwanzo mwisho.

Kabla ya kuanza kutumbuiza, Sugu aliwaambia mashabiki hao kwamba licha ya yeye kuwa mbunge wa jimbo la Mbeya mjini lakini hawezi kuacha asili yake ya kuimba muziki wa ‘Hip Pop’ kwani ndio sehemu ya maisha yake.

Alisema baada ya kufanikisha ‘Show’ aliyoifanya Jijini Dodoma, mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na ile iliyofuatia kwa wakazi wa Dodoma sasa ilikuwa imebaki burudani ya kutosha kwa wapiga kura wake wa Mbeya Mjini.

 “Ndugu zangu, niwahakikishie tu kwamba mimi ni mwanamuziki mkongwe na niliahidi nikiwa mbunge nitatumia hata jukwaa la muziki wangu ili kufanikisha utatuzi wa matatizo ya wananchi wa Jimbo la Mbeya mjini. Na leo hii niwaambie hiki kiingilio chenu kitatumika kushonea sare za wanafunzi yatima tunawao wasomesha watakaoanza kidato cha kwanza Januari mwakani.

“Lakini pia hii ni burudani yangu kwenu, kwani muda mwingine tunahitaji kufanya muziki na maisha yaendelee kama hivi. Hivyo nawashukuru sana kwa ‘Support’ yenu’” alisema Sugu


Advertisement