TCAA yafafanua kuhusu leseni ya biashara ya kampuni ya Fast Jet

Muktasari:

  • TCAA imefafanua kuhusu leseni ya biashara iliyoombwa na Fast Jet ikisema kuwa  walichelewa kuwasilisha maombi.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema kitendo cha Kampuni ya ndege ya Fast Jet kushindwa kuwasilisha kwa wakati mpango mkakati wa biashara, ndiyo sababu iliyowasababisha wakose leseni mpya ya biashara.

Johari alisema hayo jana, Jumatatu Juni 24, 2019 wakati akizungumza na Mwananchi muda mfupi baada ya kuzinduliwa kwa kongamano la pili la wadau wa sekta ya anga, lililokuwa na ajenda mbalimbali na miongoni ni ya mchango wa sekta ya anga kwenye ajenda ya kuipeleka Tanzania ya viwanda.

“Waliwasilisha siku moja kabla ya kikao cha bodi jambo ambalo lilikuwa gumu kulifanyia kazi. Ila tutalifanyia kazi katika kikao kijacho cha wadau,” alisema Johari.

Kuhusu madeni ya Sh7 bilioni waliyokuwa wakidaiwa Fast Jet, Johari alisema fedha zote zimelipwa isipokuwa maslahi ya wafanyakazi ambayo hawezi kuzungumzia kwa kuwa kesi ipo mahakamani.

Wiki iliyopita tangazo lilitolewa na TCAA katika gazeti la Mwananchi likieleza kuwa Fast Jet imeomba kufanya safari kwenye maeneo kumi pamoja na za kimataifa za Afrika Kusini, Lubumbashi, Lusaka, Kigali, Moroni na Dubai.