TEF waitaka Serikali ya Tanzania kutoa maelezo kuhusu Azory Gwanda

Muktasari:

  • Jukwaa la Wahariri (TEF) nchini Tanzania limeitaka Serikali ya Tanzania kutoa maelezo ya kina kuhusu mwandishi wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communication’s Ltd (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda aliyechukuliwa na watu wasiojulikana Novemba, 2017

Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri (TEF) nchini Tanzania limeitaka Serikali ya Tanzania kutoa maelezo ya kina kuhusu mwandishi wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communication’s Ltd (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda aliyechukuliwa na watu wasiojulikana Novemba, 2017.

TEF imetoa tamko hilo leo Alhamisi Julai 11, 2019 baada ya Waziri wa Mambo ya Nje nchini,  Profesa Palamagamba Kabudi kunukuliwa katika mahojiano kwenye kipindi cha Focus on Africa cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC)  kuhusu kutoweka kwa mwandishi huyo.

Katika kipindi hicho Profesa Kabudi amesema Azory ni miongoni mwa wananchi waliopotea na kufariki.

Azory ameacha alama kubwa; kwanza katika familia yake ambako anazidi kukumbukwa na ndani ya tasnia ya habari aliyokuwa akiifanyia kazi kabla ya kukumbwa na mkasa huo.

Kwa mujibu wa mkewe, Anna Pinoni (35), siku hiyo asubuhi watu wanne wakiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe, walifika katikati ya mji wa Kibiti, sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara, na kumchukua.

Watu hao walimpeleka hadi shambani ambako mkewe alikuwa akilima na akamuaga kuwa anaenda kazini, lakini hajarudi hadi leo.

Katika tamko hilo TEF imelitaka Jeshi la Polisi nchini Tanzania  kumtumia Profesa Kabudi katika uchunguzi kwa maelezo kuwa anaonekana ana taarifa za kutosha kuhusu Azory.

Maelezo ambayo yamedaiwa na TEF ni pamoja na Serikali kueleza Azory alikufa kifo kipi na alifia wapi.

Kingine ambacho jukwaa hilo limetaka kufahamu ni kama  mwili wa Azory ulizikwa, ulitupwa porini au uliyeyushwa kama wa mwandishi Jamal Kashogi.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na kaimu mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deodatus Balile  imehoji mahali ambapo Profesa Kabudi amepata taarifa za kifo cha Azory na haki ya familia na waandishi wa habari kumzika na kuweka matanga yake itapatikanaje.

Jukwaa hilo pia limeihoji Serikali ni watu gani waliomchukua Azory na kumuua na hatua zipi zinachukuliwa baada ya kauli hiyo ya Profesa Kabudi.

Hata hivyo, Profesa Kabudi aliyeko nchini Uingereza ametoa ufafanuzi kuhusu kauli yake hiyo, kwamba alinukuliwa nje ya muktadha.

Katika tamko lake kwa vyombo vya habari, Profesa Kabudi aliyehudhuria kongamano la uhuru wa habari nchini Uingereza juzi amesema, “Mpaka sasa hakuna uthibitisho kuwa Azory yuko hai au amefariki. Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuchunguza tukio hilo na matukio mengine yaliyotokea katika machafuko ya Kibiti, Pwani yaliyosababisha ama watu kadhaa kupoteza maisha au kupotea.”

Kwa ujumla taarifa za kutoweka kwa Azory zilitangazwa kwa mara ya kwanza Desemba 7, 2017 katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wa habari. Mkutano huo ulifanyika ofisi za makao makuu ya MCL zilizopo Tabata Relini, Dar es Salaam.

Baadaye, MCL iliendesha kampeni ya kumtangaza Azory kwenye kurasa za mbele za magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na mitandao yake kwa kipindi cha siku 100. Licha ya juhudi zote hizo, hadi Machi 1, 2018 wakati zilipotimia siku 100 hakuna taarifa iliyotolewa na chombo chochote kuhusu mahali Azory alipo, hadi leo hakuna taarifa zozote.