Taharuki mtoto mwingine akiuawa Njombe

Muktasari:

Mauaji hayo yanatokea ikiwa zimepita siku mbili tangu Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani ambaye anaongoza kikosi kazi maalumu kilichotua hapa kufuatilia matukio hayo kusema hakuna mtu aliyeshiriki kutekeleza mauaji hayo atakayebaki salama.

Njombe. Siku mbili baada ya Jeshi la Polisi kuanza operesheni ya kuwasaka wanaofanya mauaji ya watoto wilayani Njombe, juzi saa nne usiku wananchi wa Kijiji ya Matembwe walishuhudia mwili wa Rachel Malekela ukiwa umetelekezwa kichakani.

Mbali ya tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka alisema jana kuwa watu wanne wameuawa na wananchi waliowashuku kuhusika na mauaji ya watoto katika Wilaya za Njombe na Wanging`ombe.

Pia alisema mtu mwingine mmoja ameuawa na wengine watatu kujeruhiwa na wananchi katika Kijiji cha Magunguli, Mufindi mpakani na Njombe baada ya kuhisiwa kuhusika na mauaji hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William alisema watu hao waliingia kijijini hapo Januari 31 na wananchi waliwatilia shaka licha ya kuwa watu wema. Waliwekwa chini na uangalizi wa mgambo lakini wananchi walivamia na kuanza kuwapiga hadi mmoja kufariki dunia.

Katika tukio la Matembwe, mwenyekiti wa kijiji hicho, Brayson Malekela, binti huyo aliyekuwa akisoma darasa la pili Shule ya Msingi Matembwe hakuonekana nyumbani baada ya kutoka shule.

Mauaji hayo yanatokea ikiwa zimepita siku mbili tangu Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani ambaye anaongoza kikosi kazi maalumu kilichotua hapa kufuatilia matukio hayo kusema hakuna mtu aliyeshiriki kutekeleza mauaji hayo atakayebaki salama.

Jana, Malekela ambaye pia marehemu ni mtoto wa mdogo wake, alisema wazazi wa Rachel walibaini mtoto wao kutoonekana nyumbani kuanzia saa 12 jioni na kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na wananchi kuanza kumtafuta na saa nne usiku walipokuta mwili wake katika msitu uliopo kijijini hapo.

“Shingoni ni kama vile amechomwa na vitu vyenye ncha kali, pia sehemu ya shingo kwa nyuma kama amechomwa na vitu vya nchi kali na koromeo ni kama amekatwa hivi,” alisema Malekela.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri alisema aliyegundua kutoonekana Rachel ni mama yake, Petronila Nisilu baada ya kurudi nyumbani wakati baba yake, Chelio akiwa bado kazini.

“Mtoto huyu alikuwa na mama yake shambani, alimwambia mwanaye awahi kurudi nyumbani kwa ajili ya shughuli za nyumbani, aliporudi hakumkuta ndipo alipomwambia mumewe na kuanza harakati za kumtafuta,” alisema.

Alisema saa nne usiku kundi moja kati ya yaliyokuwa yamegawanywa walikuta mwili wake kwenye msitu huo akiwa ameshafariki na majeraha shingoni.

Mkazi wa Kitongoji cha Mtakuja kijijini hapo, Edigood Mtewele alisema yeye na wenzake walikuwa kwenye sungusungu muda wa jioni wakapewa taarifa hizo na wakaanza safari ya kuungana na wenzako kumtafuta mtoto huyo.

“Tuna sungusungu kwa muda mrefu, lakini baada ya kuibuka kwa matukio haya maeneo mengine, tulilazimika kuongeza nguvu ya doria kukagua magari ili kujiridhisha watu wanaoingia na kutoka eneo hili,” alisema Mtewele. Msafiri aliyeongoza mazishi ya mtoto huyo jana jioni alisema Njombe ipo kwenye kipindi kigumu kutokana na mauaji ya watoto yanayoendelea.

“Serikali imeshatuma kikosi kazi kuchunguza matukio haya na kimeanza kazi. Hatukutarajia kama tukio hili lingetokea wakati kazi imeanza, inauma sana,” alisema.

“Damu ya huyu mtoto haitapotea bure, itawatafuna wale wote waliohusika na unyama huu, lakini pia Serikali haitalala. Muda wote tupo kazini na hadi sasa kuna watu wanashikiliwa kuhusiana na tukio hili,” alisema.