Taka unazotupa chanzo cha mkaa

Wadau wa mazingira wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alipokuwa  akizungumza kwenye mjadala wa Jukwaa la Fikra uliojadili matumizi ya mkaa, uchumi na mazingira yetu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis

Muktasari:

Akizungumza katika mdahalo wa Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi, mkurugenzi wa Kampuni ya Kuja na Kushoka, Leonard Kushoka alisema kampuni hiyo inatumia takataka za aina mbalimbali kutengeneza mkaa mbadala ambao unasaidia kuokoa mazingira kwa kuzuia ukataji miti hovyo.

Taka unazitupa, ni malighafi muhimu ya kutengeneza mkaa mbadala kwa kampuni ya Kuja na Kushoka Tools Manufactures Group ambayo imekusudia kutafuta chanzo kingine cha nishati kuokoa miti inayokatwa hovyo hivyo kuchangia kupungua kwa misitu.

Hilo limebainishwa na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Leonard Kushoka kwenye mdahalo ulioandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuzungumzia masuala ya mkaa, nishati na mazingira ili kutafuta suluhisho la kudumu.

Kwenye mjadala huo uliofanyika Februari 7, Kushoka alisema kila changamoto inayojitokeza huiona kuwa ni fursa ya maendeleo na hivyo ndivyo ilivyokuwa katika suala la ukataji miti.

Anasema ni vigumu kumhamisha mtu kuachana na matumizi ya mkaa na kutumia gesi au umeme lakini ni rahisi kumhamisha kutumia mkaa mbadala.

“Mungu alinipa kipaji cha ubunifu, niliangalia nifanye nini kuhakikisha teknolojia inakidhi kuwa matumizi ndipo tuliweza kubuni mashine,” anasema.

Kwa kuzingatia hatua za kuchoma mkaa ambazo hujumuisha kujenga matanuri, kuweka miti, kuwasha moto na kufunika kwa udongo kuzuia kiwango cha hewa ya oksijeni inayoenda ndani na kutunza joto kabla ya kupata mkaa.

Baada ya kutembelea na kujionea mkaa unavyoandaliwa, anasema walijiuliza kwa nini watu wanachoma kuni nyingi na wanapata mkaa kidogo huku uvunaji huo wa miti ukisababisha uharibifu wa mazingira ndipo wakapata cha kufanya.

Mkaa mbadala

Kupata mkaa mbadala, Kushoka anasema anahitaji mabaki ya mimea mfano maranda ya mbao, maganda ya karanga, pumba hata majani ya mpunga.

Mabaki hayo, anasema yanapatikana kwa wingi mkoani Tabora ambako ndiko ofisi yake ilipo ingawa hata kwenye majiji kama Dar es Salaam, Mbeya au Arusha si tatizo kupata malighafi zifaazo.

Mfano jijini Dar es Salaam, Kushoka anasema mabaki ni mengi hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kuachana na matumizi ya mkaa wa kawaida na kutumia mkaa mbadala kiasi cha kuokoa ukataji miti na kutunza pia mazingira.

“Wasimamizi wa mazingira wanasema Dar es Salaam inakusanya zaidi ya tani 6,000 za takataka kwa siku. Kati ya taka hizo, asilimia 60 ni mabaki ya mimea na mazao kwa hiyo watu wakipata elimu ya uzalishaji mkaa mbadala…taka zitakuwa mali,” anasema.

Anasema watu watapata ajira kupitia kazi hiyo kama ilivyo kwa chupa za plastiki, hivyo bidhaa ya mkaa mbadala ikiungwa mkono na Serikali na kuhamasishwa vya kutosha itaondoa hali ya uchafu katika jiji hilo.

“Asilimia 60 ya taka za Dar es Salaam ni mabaki vya mazao yanayouzwa sokoni kama ndizi, mahindi, viazi ambayo yanatosha kuzalisha mkaa kila siku. Tunafikiria kuweka kambi dampo ambako takataka zote zinapelekwa ili kuzikusanya kwa urahisi,” anasema Kushoka.

Afya

Kupata mkaa mbadala wenye ubora, anasema mtengenezaji anahitaji kuzingatia maandalizi anayoyafanya suala ambalo hufanyika hata kwenye uchomaji wa mkaa wa kawaida.

Kwenye uchomaji mkaa wa kawaida, mtu anahitaji miti ambayo akichoma kuna sumu inabaki mule tofauti na inavyokuwa kwenye maandalizi ya mkaa mbadala unaotumia mabaki ya mimea ambayo hujumuisha vitu vidogo vidogo ambavyo vikichomwa kwenye tanuru vinaungua na kubaki vumbi jeusi.

Vumbi hili ndilo hutumika kutengenezea mkaa mbadala, hii ni baada ya sumu zote kuwa zimeondoka ambazo hata baada ya matumizi ya muda mrefu, mtumiaji hawezi kupata athari za kiafya kama maradhi ya kifua.

Kupatikana kwa vumbi hilo ambalo huchanganywa na gundi ambayo kwa kawaida, wao hutumia udongo mfinyanzi na kukoroga kwa pamoja. Kugundisha vumbi la mabaki yaliyochomwa, unaweza kutumia unga wa muhogo uliochanganywa na maji.

“Hivi sasa tumeenda mbali zaidi, tunatumia udongo mfinyanzi kama gundi, hatuchanganyi kitu chochote chenye kemikali. Tunachukua vumbi na uji wa udongo wa mfinyanzi na kuvichanganya kwenye mashine tuliyobuni wenyewe kupata mfano wa vitofali kisha tunavianika juani,” anasema Kushoka.

Gharama nafuu

Wakati gunia la mkaa wa kawaida ni Sh50,000 hadi 70,000 kwa Dar es Salaam hivyo kilo moja huuzwa kati ya Sh1,000 hadi 1,500 lakini anasema mkaa mbadala ni mzito na bora kuliko wa miti, bei yao kwa kilo inaanzia Sh 2,000.

Anasema uwakaji wa mkaa mbadala ni kati ya saa tatu hadi nne kwa jiko la kilo moja linalomuwezesha mama kuivisha vyakula vyote bila kuongeza mkaa hivyo kupunguza kiasi kinachotumika ikimaanisha fedha kidogo zinatumika kwa kila familia au kaya.

Kwa hesabu zake, anasema kilo moja ya mkaa mbadala ni sawa na kilo nne hadi tano za mkaa wa miti.

Mashine za mkaa

Kampuni ya Kushoka inaunda mashine za uchomaji mkaa mbadala ikiwa na wafanyakazi 14 walio kazini muda wote.

Kukamilika kuundwa kwa mashine husika ni hatua moja kati ya tatu kabla mkaa mbadala haujapatikana. Kinachofuata ni kutafuta wateja ambao wakishalipia hufundishwa na kuitumia mashine husika.

Kulingana na malighafi zitakazotumika kuandaa, mashine hizo zina uwezo tofauti. Anasema zipo zinazoweza kuzalisha hadi tani tatu kwa siku ikisimamiwa na watu wasiopungua watano ambayo huuzwa Sh15 milioni.

“Tunazo za Sh3 milioni ambazo huzalisha kati ya kilo 30 hadi 50 kwa siku, yenye uwezo wa kuzalisha kilo 800 hadi 1,500 tunaiuza Sh8 milioni,” anasema.

Kwa malipo utakayofanywa, kampuni yake inakufungia mashine husika, inakufundisha kuitumia na kukuhakikishia soko ikinunua mkaa utakaochoma kwa bei ya jumla ili wao wauuze kwa bei ya rejareja.

Licha ya kampuni hiyo, mashine za kuchoma mkaa mbadala zikiagizwa kutoka nje hasa Canada, India na China ile ambayo wao huiuza Sh15 milioni, hugharimu zaidi ya Sh25 milioni.

“Tutazisambaza nchi nzima ingawa kwa sasa tumeanza na Dar es Salaam kwa kuwa kuna mahitaji makubwa ya mkaa,” anasema.

Kwenye maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Mei 31 mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema teknolojia ya uzalishaji mkaa mbadala ikuzwe na kusambazwa kote nchini kuwawezesha wananchi kuachana na matumizi ya mkaa wa kawaida kwa lengo la kuhifadhi misitu na kupunguza uharibifu wa mazingira.

Takwimu zilizopo zinaonyesha Dar es Salaam inatumia tani 500,000 za mkaa kwa mwaka hivyo kuongoza ikilinganishwa na mikoa mingine nchini.

Akieleza faida za mkaa mbadala na majiko wanayotengeneza, Kushoka anasema ikiwa Dar es Salaam ilikuwa inatumia tani 2,000 za mkaa kwa siku, basi itatumia tani 1,000 za mkaa mbadala hivyo itaokoa mazingira.

Changamoto

Kuja na Kushoka ambao ni washindi katika shindano la mkaa mbadala lililoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, anasema kuna mengi walipanga kuyafanya lakini wamekwama kutokana na fungu waliloahidiwa kutotekelezwa kwa wakati.

Anasema Ofisi ya Makamu wa Rais ilisimamia tuzo walizoshinda na mradi ulikuwa ni wa Sh300 milioni lakini wanapata Sh50 milioni kila baada ya miezi sita sawa na asilimia 16 kwa kipindi cha miaka mitatu linalowafanya washindwe kujitanua.

“Malengo yetu yanatutaka mwaka huu tutengeneze mashine 300 lakini hatuwezi kutengeneza hizo zote kama hatuna mtaji wa kutosha. Hivi sasa tunatengeneza mashine 10 ambazo tunaziingiza sokoni zikiisha tunatengeneza nyingine 10, tunaenda hivyo hivyo,” anasema.

Mbali na hayo, Kushoka anaishauri Serikali kufanya uamuzi mgumu ili kufikia malengo ya kuachana na matumizi ya mkaa wa kawaida.

Anasema kuna kipindi Serikali ilitishia kusitisha ukataji miti sababu ya mkaa na wakati huo zaidi ya mashine 50 zilinunuliwa.