Takukuru Tanga, Kinondoni zilivyonusa harufu ya rushwa

Muktasari:

  • Mkuu wa Takukuru mkoa huo, Christopher Mariba alisema hayo juzi wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi mwaka 2019.

Tanga. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Tanga imesema uzembe wa baadhi ya viongozi katika usimamizi na uhamasishaji wananchi umechangia kuwapo kwa dosari katika miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri za mkoa huo.

Aidha, Takukuru mkoa wa Kinondoni imebaini kuwa baadhi ya watumishi wa umma ni miongoni mwa watu wanaodaiwa kushiriki vitendo vya kupokea na kuomba rushwa katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.

Mkoani Tanga taasisi hiyo imeanza kuwachunguza waliosababisha hali hiyo na kisha kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ikiwamo kuhakikisha wanalipa hasara waliyosababisha.

Mkuu wa Takukuru mkoa huo, Christopher Mariba alisema hayo juzi wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi mwaka 2019.

Alisema katika kipindi hicho wamefanya ufuatiliaji wa miradi 30 iliyo katika sekta za maji, afya, ujenzi na elimu inayotekelezwa kwenye halmashauri za mkoa huo.

Alisema dosari nyingi zenye kuashiria kuwapo kwa mianya ya rushwa zimeonekana kwenye utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu na majengo yaliyopo kwenye sekta ya elimu na maji.

Alisema katika kipindi hicho, Takukuru mkoani humo imeokoa Sh 2,190,500 zilizokuwa zimechukuliwa kinyume cha sheria na taratibu za fedha ikiwamo watumishi kujilipa kiasi kikubwa cha posho ikilinganishwa na safari zilizofanyika.

Wakati huohuo, Bakari Kiango anaripoti kuwa, Takukuru mkoa wa Kinondoni imebaini kuwa baadhi ya watumishi wa umma ni miongoni mwa watu wanaodaiwa kushiriki vitendo vya kupokea na kuomba rushwa katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.

Mkuu wa Takukuru mkoa huo, Theresia Mnjagira alisema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi wa taasisi hiyo kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.

Alisema katika kipindi hicho wamewafikisha mahakamani watumishi wa umma wa tano kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ili watoe huduma kwa wananchi.