Takukuru yamruka Zitto

Muktasari:

Zitto alidai kuwa kitendo cha Takukuru kumuingiza katika mfumo wa Uhamiaji ili azuiliwe kusafiri nje ya nchi ni ukiukwaji wa Katiba.


Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Brigedia Jenerali John Mbungo alisema taasisi hiyo haijamuagiza mtu au taasisi yoyote kumkamata na kumhoji Kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe.

Awali, Zitto alidai kuwa kitendo cha Takukuru kumuingiza katika mfumo wa Uhamiaji ili azuiliwe kusafiri nje ya nchi ni ukiukwaji wa Katiba.

Juzi, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini alikwama kwenda Kenya akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Aman Karume, Zanzibar.

Zitto alikutana na kadhia hiyo juzi mchana baada ya kushikiliwa kwa muda na Idara ya Uhamiaji kabla ya kuachiwa usiku.

Msemaji wa Uhamiaji Zanzibar, Sharif Bakar Sharif alisema jana kuwa kilichofanywa hatua ya kumzuia mwanasiasa huyo ni kutekeleza agizo la Serikali kwa mujibu wa taratibu za vyombo vya ulinzi na usalama.

“Sisi kwa kuwa ni sehemu ya vyombo vya ulinzi na usalama, tulitekeleza agizo hilo la kutomruhusu kusafiri nje ya Tanzania na tayari tumeshamfikisha katika vyombo vingine vya sheria kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria na kikanuni,” alisema Sharif bila kueleza kwa undani agizo hilo la Serikali limetolewa na nani.

Zitto aliwaambia waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho Vuga Mjini Unguja kwamba Takukuru ndio iliyotoa amri ya kuzuiwa kusafiri.

Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amewekewa zuio la kutosafiri nje ya nchi na mamlaka za Serikali.