Tani 200 za mifuko ya plastiki zakusanywa Dar, kilo 500 Arusha

Dar/Mikoani. Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (Nemc) limesema zaidi ya tani 200 za mifuko ya plastiki zilikuwa zimesalimishwa mkoani Dar es Salaam hadi jana.

Pia, limesema vifungashio vya plastiki ambavyo havijapigwa marufuku vitaendelea kupatikana na kuzalishwa nchini.

Wakati Dar es Salaam ikikusanya kiasi hicho, Arusha imekusanya kilo 500 kutoka katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa Wiki ya Mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo, Ofisa Mkaguzi wa Mazingira wa NEMC, Lilian Kapakala alisema mwitikio wa watu na usalimishaji wa mifuko hiyo ni mkubwa na unaendelea.

Aliwaambia washiriki wa mkutano huo kuwa vifungashio ambavyo havijapigwa marufuku vitaendelea kupatikana akitolea mfano wa vile vya vyakula.

“Plastiki zote zina madhara, lakini sasa tunaenda katika uchumi wa viwanda, hatuwezi kuzuia vifungashio vyote vya plastiki bila kupata mbadala wake, lakini kwa kuanza, tumeanza na mifuko ya ‘rambo’,” alisema.

Katika mkutano huo, Mkuu Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori alisema ingawa marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki ina nguvu ya kisheria, inahitaji uhamasishaji kwa wananchi na kuwaeleza madhara ya mifuko hiyo na faida za kuacha kuitumia sanjari na kuwaeleza njia mbadala.

“Mifuko hii haiozi kama taka zingine, lakini pia inaziba mitaro na mifereji ya maji machafu na kusababisha magonjwa ya milipuko, hivyo marufuku hii inalenga kutunza mazingira,” alisema Mkori.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Beatrice Dominic alisema ofisi yake imezungumza na mkandarasi anayekusanya taka na kukubaliana kutenganisha mifuko ya plasitiki na taka nyingine zinazoweza kuoza.

Alisema wilaya hiyo imetenga vituo zaidi ya 14 kwa ajili ya kukusanya mifuko inayosalimishwa.

“Natoa wito kwa watu kusalimisha mifuko hiyo katika vituo vilivyopo kwenye kila kata, wasichanganye mifuko na taka nyingine ... tutaendelea kutoa elimu kwa siku 30 mfululizo kuanzia kesho ili watu waelewe,” alisema.

Fursa yapatikana

Marufuku ya mifuko ya plastiki inayoanza leo imekuwa fursa na changamoto. Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi jana ulibaini kuwa viwanda vinavyozalisha mifuko mbadala vimeongeza uzalishaji wake kwa lengo la kukidhi mahitaji.

Aprili 10, akiwa bungeni Dodoma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza marufuku hiyo akisema jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kutengeneza, kuuza, kuingiza na kutumia mifuko hiyo.

Ili kutekeleza agizo hilo, waziri mwenye dhamana ya Mazingira, Januari Makamba alitoa ufafanuzi akisema siyo mifuko yote ya plastiki itakayopigwa marufuku, na kwamba baadhi ya vifungashio vya plastiki vitaendelea kutumika kama vya dawa za binadamu, pembejeo za kilimo, vya viwandani, ujenzi na vya maziwa.

Jana, mkoani Dar es Salaam, watu wengi walionekana wakiuza na kununua mifuko mbadala katika maduka ya jumla.

Muuza mifuko aliyekutwa akinunua vibebeo hivyo katika dukalililopo Kariakoo, Omary Njoli alisema, “ninauza zaidi mifuko mbadala kuliko hii ya plastiki. Hii ya plastiki hapa ninayo miwili tu, kwenye maduka ya jumla haipatikani sasa hivi tunauziwa hii.”

Mkoani Kilimanjaro

Huko nako zuio la mifuko hiyo limeanza kutekelezwa. Wenye mabucha hasa maeneo ya vijijini na pembezoni mwa mji wameanza kutumia magazeti kuwafungia nyama wateja wao.

Baadhi ya wamiliki wa mabucha hayo wameliambia Mwananchi kuwa wanalazimika kugeuza magazeti kuwa vibebeo kwa sababu hawawezi kumudu bei ya mifuko mbadala iliyoruhusiwa.

“Huku mitaani unakuta mtu anakuja kununua nyama robo kilo utamfungia kwenye mfuko wa Sh200? Mifuko ya plastiki ilikuwa afadhali (Sh50),” alisema mmoja wa wamiliki wa bucha.

Hata hivyo, mkazi wa Tarakea, Rombo, Yusuph Mruma aliitaka Serikali kuingilia kati na kupiga marufuku matumizi ya magazeti katika kufungia nyama akisema si salama kwa afya ya mlaji.

Kuhusu hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira aliagiza wenye mabucha wote kutumia mifuko mbadala, “ninaelekeza wenye mabucha wote wawafuate wazalishaji wa mifuko ya khaki inayozalishwa hapa mkoani na waache mara moja kutumia magazeti.”

Kuhusu kuingia sokoni kwa mifuko mbadala yenye malighafi ya plastiki, kama ilivyodaiwa na baadhi ya wakazi wa Moshi, Mghwira alitoa wito kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kubainisha viwango vinavyokubalika.

Alisema Serikali ya mkoa imechukua hatua ya kukusanya mifuko yote ya plastiki iliyozagaa kwenye maeneo mbalimbali.

Aliwataka wenye idadi kubwa ya mifuko ya plastiki hasa wenye maduka na supermakert kuisalimisha kwenye ofisi za halmashauri.

Hali ilivyo Arusha

Jana, wafanyabiashara wakubwa wa mifuko hiyo walisalimisha kwenye ofisi za kata na dampo zaidi ya kilo 500.

Hata hivyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda ambaye yupo katika ziara mkoani humo aliwaondoa hofu wananchi kuwa hakutakuwa na uhaba wa vibebeo kwa sababu Serikali imejipanga.

“Jana nimetembelea kiwanda cha Hasho, kilichopo Hai, Kilimanjaro, wanazalisha mifuko takriban 680,000 kwa siku, hivyo kuna mifuko ya kutosha, asije akatokea mtu akaanza kugombana na Serikali kwa kudhania kuna uhaba wa mifuko,” alisema.

Ofisa masoko wa kiwanda cha Green Earth kinachotengeneza mifuko mbadala ya karatasi kilichopo Dar es Salaam, Jonesia Sebastian alisema wiki yote hii, mashine zao hazijapata muda wa kupumzika.

Hata hivyo, juzi meneja wa Hasho, Joseph Njalu, alisema kiwanda chao kina uwezo mkubwa lakini kinakabiliwa na changamoto ya uingizwaji wa mifuko bandia inayofanana na wanayozalisha.

Mkoani Mbeya

Jana, wafanyabiashara wa mifuko ya plastiki waliitikia wito wa Serikali wa kusitisha kuuza mifuko hiyo na ambayo si rafiki kwa mazingira.

Mwananchi ilishuhudia wafanyabiashara wadogo machinga wakiiuza licha ya kulalamikia bei kubwa wanayouziwa kwenye maduka ya jumla wakisema hawapati faida.

“Unajua mtu akinunua mfuko huu wakati mwingine akitaka kuja sokoni anakuja nao tena, tofauti na mifuko ya plastiki ambayo ilikuwa inauzwa kwa Sh100, hii mbadala inauzwa kwaSh300 hadi Sh500,” alisema Christopher Ezekia.

Imeandikwa na Ephrahim Bahemu, Daniel Mjema, Janet Joseph, Rachel Chibwete, Yonathan Kossam, Mussa Juma na Teddy Kilanga.