Tanzania yatoa msaada wa chakula, dawa Malawi, Msumbiji na Zimbabwe

Askari wa JWTZ wakipakia dawa na Chakula kwenye Ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam leo ikiwa ni msaada uliotolewa na Serikali kwa ajili ya watu waliokumbwa na Kibunga  Malawi, Msumbiji na Zimbabwe. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Kufuatia Kimbunga cha Idai nchini Malawi, Msumbiji na Zimbabwe ambacho hadi sasa inasemekana watu takribani 1,000 wamepoteza maisha, Rais John Magufuli ametoa msaada wa tani 214 za chakula na dawa tani 24.


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetoa msaada wa chakula na dawa kwa nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe kufuatia Kimbunga cha Idai ambacho hadi sasa inasemekana watu takribani 1,000 wamepoteza maisha na shughuli za uokoaji zinaendelea.

Msaada uliotolewa ni dawa za binadamu tani 24, mchele tani 14 na mahindi tani 200, hata hivyo thamani yake haijatajwa.

Leo Jumanne Machi 19, 2019 Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wamekabidhi msaada huo kwa mabalozi wa nchi hizo nchini, kisha ikaanza kupakiwa katika ndege ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kuisafirisha.

Profesa Kabudi amesema misaada hiyo imetolewa na Rais wa Tanzania, John Magufuli baada ya kupata taarifa za kimbunga kisha kuongea na maraisi wa nchi hizo kujua hali halisi.

"Sisi tuna wajibu na vifo vya jirani zetu, shida za majirani zetu ni za kwetu leo kwao kesho kwetu. Huu ni msaada wa Serikali lakini tunatoa wito kwa watu binafsi, mashirika na kampuni nchini kuwachangia hao majirani zetu kupitia ofisi ya Waziri Mkuu," amesema Profesa Kabudi.

Waziri Mwalimu amesema alipokea maelekezo kutoa kwa Rais Magufuli kuandaa msaada huo hivyo kila nchi itapata tani 8 za dawa.

"Baada ya maelekezo ya Rais, niliongea na mawaziri wenzangu wa afya wakanieleza dawa wanazohitaji wote waliniambia wanahitaji dawa za kuzuia maambukizi ya bakteria na magonjwa ya matumbo hivyo kwa asilimia kubwa ndizo tulizowapatia," amesema.

Ameongeza Serikali iko tayari kutoa msaada wa madaktari watakaoongeza nguvu katika utoaji wa huduma za afya katika nchi hizo kwa kipindi hiki.