UCHOKOZI WA EDO: TRA imerudisha mashairi mazuri katika bendi zetu

Ilitokea wiki chache zilizopita. Nikavamia baa moja pale Tabata usiku wa manane. Bendi ya Twanga Pepeta ilikuwa ikitumbuiza. Inajaribu kurudisha nyuma nyakati. Nikakumbuka wakati ule ikiwa katika ubora wake, ilitamba sana.

Kuna watu walikuwa wanatamba sana nje ya jukwaa. Walikuwa wanaitwa mapedeshee (PDG). Ghafla nikakumbuka kuwa siku hizi hawaimbwi. Majina yao hayatajwi. Zamani wakati DDC Mlimani Park na Msondo Ngoma wakitamba hakukuwa na utaratibu wa kutaja majina ya watu wenye fedha ndani ya wimbo.

Enzi za akina Marijani Rajab ulihitaji kufanya kituko kama yule Masoud aliyemuimba ili utajwe au utungiwe wimbo. Fedha zako zilikuwa hazisaidii kuimbwa na mtu kama Marijani labda kama ulifanya kituko cha aibu.

Kizazi kipya cha dansi ndicho kilileta tabia ya kutaja watu maarufu na wenye fedha katika nyimbo. Iliondoa ladha, lakini tungefanya nini? Wao ndio walikuwa wafadhili wa wanamuziki. Zamani enzi za kina Mbaraka Mwinshehe hata ungekuwa na fedha kiasi gani hautajwi. Zilipokuja zama za kina Twanga Pepeta ndipo ulipoanza utaratibu huu.

Wanamuziki badala ya kujikita katika tungo za mashairi mazuri wakajikita katika kutajataja majina ya watu wenye fedha. Nilichoshuhudia Tabata ni kwamba mashairi mazuri yanaanza kurudi. Majina hayatajwitajwi. Wenye fedha siku hizi wanaogopa kutajwa majina.

Nikauliza, kisa? Jibu lake likaja na herufi kubwa tatu tu. TRA. Nikapewa kisa kizima. Siku hizi ukitajwatajwa tu na bendi maofisa wa TRA wapo mgongoni kwako. Ukienda mbele kutuza wanamuziki maofisa wa TRA wapo na wewe.

Maofisa watataka kujua kama unalipa kodi na unafanya biashara zako kihalali, lakini zamani hata wafanyakazi wa Serikali nao walikuwa wanaimbwa. Nao walijigeuza ‘Ma-CEO’ katika ofisi zao hata kama walikuwa ni makarani wa kawaida. Sasa Namba Moja ameziba mirija wamekimbia katika kumbi.

Hakuna anayetaka kutajwa katika nyimbo. Wanamuziki wanajaribu kutunga mashairi mazuri ili wawateke wasikilizaji. Majina yamepungua. Haikuwa hiyari yao, lakini hakuna wanachoweza kufanya zaidi ya hapo. Ghafla Anko amelazimisha tuingie katika utaratibu mwingine wa kuheshimu fedha na nafasi zetu za biashara na kazi. Maisha yanaenda kasi sana.