UFISADI: Mradi wa Sh15 bil katika uchunguzi

Friday January 18 2019Mkuu wa Takukuru mkoa wa Geita,

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Geita, 

By Rehema Matowo, Mwananchi

Geita.Takukuru mkoani Geita imeunda kamati ya kuchunguza mradi wa maji wa Nyamtukuza wilayani Nyang’hwale kutokana na kujengwa zaidi ya miaka mitano bila kukamilika.

Mradi huo unaojengwa kwa gharama ya Sh15 bilioni uliondolewa mikononi mwa halmashauri hiyo Novemba mwaka jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kurudishwa wizarani lakini bado unasuausa huku vijiji zaidi ya 17 vikiwa havina maji vikitegemea kukamilika kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita, mkuu wa Takukuru mkoa wa Geita, Thobias Ndaro alisema kamati hiyo ina siku tatu tangu ianze kazi na inategemewa kukamilisha mwezi huu mwishoni.

“Tumeunda kamati kuchunguza mradi huo wa maji kwa kuwa haujakamilika muda mrefu sasa, wamepita viongozi wengi wakiwamo mawaziri hadi Waziri Mkuu lakini bado una tatizo na kama mlivyomsikia Waziri Mkuu una harufu ya rushwa,” alisema.

Akizungumzia miradi mingine, Ndaro alisema taasisi hiyo inaendelea kuchunguza miradi inayojengwa kwa fedha za Miradi ya Jamii (CSR) wakiwamo watumishi wa Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) ambao mkuu wa mkoa huo aliagiza kuzuiwa kwa hati zao za kusafiria na kuchunguzwa.

Alisema uchunguzi huo ukikamilika na ikibainika kuna ubadhirifu sheria itachukua mkondo wake na endapo watakua hawana kosa Takukuru itaishauri Serikali .

Alisema kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa Sh16 milioni kutoka TRA, idara ya elimu na polisi.

Aidha, Ndaro alisema Takukuru inafuatilia fedha za miradi yenye thamani ya Sh10 bilioni katika halmashauri za Geita, Chato na Bukombe ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Advertisement