Uchaguzi serikali za mitaa, Lugola avionya vyama vya siasa Tanzania

Muktasari:

  • Tanzania inafanya uchaguzi wa serikali za mitaa Oktoba mwaka 2019 ambapom Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo, Kangi Lugola ametoa onyo kwa vyama vya siasa kutojihusisha na uvunjifu wa amani kwani watachukuliwa hatua kali.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola, amesema Jeshi la Polisi litahakikisha linawashughulikia wanasiasa watakaojaribu kuwashawishi wananchi kufanya fujo kwa lengo la kuvuruga uchaguzi wa serikali za mitaa.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha habari cha wizara hiyo kimesema Waziri Lugola ameyasema hayo leo Jumatano Julai 17, 2019 wakati anazungumza na wananchi wa Mji wa Kibara, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara.

Lugola ambaye ni mbunge wa Mwibara amesema kisitokee chama chochote cha siasa kitakachojaribu kuvuruga uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 2019 ambao Watanzania wengi wamejipanga kufanya uchaguzi huo kwa amani na utulivu.

Amesema wananchi wajiepushe kudanganywa au kutumbukia katika mtego wowote wa wanasiasa.

“Wizara yangu kupitia Jeshi la Polisi haitakuwa tayari kuona na kumuacha raia wa Tanzania au asiye raia akijihusisha na vitendo vya kuhujumu uchaguzi au kuleta fujo, atadhibitiwa bila kujali nafasi yake, au uwezo wake kiuchumi,” amesema

“Hii Serikali siyo ya kuchezewa, hivyo natuma salamu kama mlikuwa na mawazo hayo yaondoeni, hatutamuonea mtu huruma ambaye ana lengo la kuvuruga amani yetu,” amesema Lugola.

Pia Waziri Lugola alivitaka vyama hivyo viwe na uzalendo na nchi yao na pia viwe na itikadi na malengo ya kisiasa ambayo hayaleti fujo kwa kufuata sheria za nchi. 

Aidha, Lugola kwa mara nyingine alizungumzia uhalifu katika ziwa Victoria, akiwataka Polisi waongeze kasi kwa kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo hayo ya ziwa kwa lengo la kudhibiti uhalifu huo.

“Huu uhalifu katika ziwa Victoria utashughulikiwa, hii ni awamu ya tano ambayo inaongozwa na Rais John Magufuli, hivyo tunataka wananchi muishi katika nchi yenu kwa amani na utulivu,” amesema Lugola.

Waziri Lugola anaendelea na ziara jimboni kwake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kufanya mikutano ya hadhara akisikiliza kero za wananchi jimboni humo na pia kuiongoza ligi yake, Kangi Bomba ambayo inashirikisha wananchi jimboni humo kufanya mashindano ya mpira wa miguu, pete, pamoja na michezo mbalimbali.