Uchunguzi alipo Mdude Chadema waendelea

Muktasari:

Kamanda wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alisema Haonga aliachiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti.

Dodoma/Dar. Wakati polisi mkoani Songwe wakieleza kuwa wanaendelea na uchunguzi kujua alipo mwanachama wa Chadema, Mdude Nyagali maarufu kwa jina la Mdude Chadema, mbunge wa chama hicho, Pascal Haonga amesimulia alivyokamatwa na polisi nje ya geti la kuingilia bungeni.

Akizungumza na Mwananchi jana, kamanda wa polisi wa Mkoa wa Songwe, George Kyando alisema bado hawajapata taarifa zozote kuhusu Mdude aliyetekwa Jumamosi iliyopita akiwa ofisini kwake Vwawa, Mbozi mkoani humo, lakini wanaendelea kufanya uchunguzi kuwabaini waliomteka.

“Tunaendelea kufanya uchunguzi, ila bado hatujawapata walioshuhudia maana wao wanaweza kutupa mwanga kidogo, ila hatujatulia tunafanya uchunguzi,” alisema Kyando.

Juzi bungeni, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni alisema polisi imefungua jalada la uchunguzi wa tukio hilo na kuongeza nguvu kutoka makao makuu ya jeshi hilo.

Chadema imelitaka jeshi hilo kuchunguza kutekwa kwa mkufunzi huyo wa ‘Chadema ni Msingi’ na kuwachukulia hatua waliohusika.

Wakati kitendawili cha alipo Nyagali kikiwa hakijateguliwa, mbunge wa Mbozi ambaye alikamatwa juzi na kuachiwa kwa dhamana jana akitakiwa kuripoti polisi kesho, amesema akiwa anatoka nje ya viwanja vya Bunge alikuta gari aina ya Land Rover 110, maarufu kama Defender, ya polisi ikiwa na askari takriban wanane na alipoegesha gari lake kulikuwa na idadi kama hiyo ya askari.

Alisema baada ya kufika kituoni alielezwa kuwa kuna makosa ya kimtandao ameyafanya mkoani Songwe, lakini baadaye walimwambia kuwa alifanya kosa hilo katika kundi la WhatsApp la wabunge mwaka jana.

Alisema kuwa jana asubuhi walikwenda naye nyumbani kwake kufanya upekuzi na aliporudishwa polisi walimpa dhamana na kumtaka kurejea kesho asubuhi. Lakini alisema simu yake imechukuliwa na polisi.

Kamanda wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alisema Haonga aliachiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti.

Jana asubuhi mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika alitaka Bunge lijadili kukamatwa kwa Haonga akisema ni kinyume na mwongozo wa Spika Job Ndugai kuhusu polisi kuwakamata wabunge wakati mkutano ukiwa unaendelea.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga alisema hoja hiyo haiwezi kukubaliwa kwa sababu Ndugai hana mamlaka hayo.

Mwananchi lilipozungumza na Ndugai kuhusu jambo hilo na majibu ya Giga, alisema ufafanuzi uliotolewa na mwenyekiti huyo unatosha.