Uchunguzi wabaini sababu za kutokoma kwa ajali za barabarani

Basi la Majinjah baada ya kuangukiwa na lori wilayani Mufindi, Iringa lilipokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam.

Muktasari:

  • 50 Idadi ya watu waliofariki katika ajali iliyotokea Mafinga kwenye basi la Majinjah Machi 11 mwaka huu.
  • 70 Idadi ya watu waliofariki katika ajali ya basi la No Challenge mwaka 1998.
  • 1996 Mwaka ambao ilitokea ajali ya Mv Bukoba na kuua watu zaidi ya 1000.

Dar es Salaam. Ajali za vyombo vya usafiri wa majini na barabarani huenda zikaendelea kutokea nchini na kuchukua uhai wa watu wengi zaidi kila kukicha kutokana Serikali kuwaadhibu madereva tu na kuwaacha maofisa waliohusika na miundombinu mibovu na wanaoshindwa kukagua ipasavyo vyombo hivyo.

Kila zikitokea ajali za barabarani, Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani hukimbilia kuwakamata madereva na kuwafungulia mashtaka na wakati mwingine wamiliki wa vyombo hivyo, lakini siyo maofisa waliosababisha barabara kujengwa chini ya kiwango, nyembamba au kuacha mashimo bila kuyafukia wala maofisa wanaoacha kukagua magari.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi, kwa muda mrefu sasa, unaonyesha kwamba, Serikali imekuwa ikishituka tu wakati wa vifo na viongozi wakihudhuria mazishi ambako hutoa makaripio na ahadi ya kuwachukulia hatua madereva wanaodaiwa kuwa wazembe na kuwawajibisha watendaji wote ambao hawafanyi lolote kuzuia majanga ya ajali. Lakini huwa hakuna ufuatiliaji, hata kesi zikitupwa, Serikali huishia kuahidi kukata rufaa bila utekelezaji.

Kwa ajali za barabarani, Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani hukimbilia kuwakamata madereva na kuwafungulia mashtaka, lakini wanaosababisha vifo katika matukio kama ya milipuko ya mabomu au kuacha nyaya za umeme zikiwa zimelala barabarani hadi kusababisha ajali hawachukuliwi hatua ambayo ni sawa na waliosimamia ujenzi wa barabara nyembamba.

Takwimu za vifo

Wakati dawa ya kudhibiti ajali haijapatikana, takwimu za Usalama Barabarani zinaonyesha kuwa mwaka 2012 kulikuwa na ajali 11,438 zilizosababisha vifo vya watu 4,919; mwaka 2013 idadi ajali ilikuwa 11,311 zilizosababisha vifo vya abiria 1,739 na mwaka jana ajali zilikuwa 8,405 na vifo vilikuwa 1,743.

Kila vinapotokea vifo vya watu kutokana na ama kulipuliwa na mabomu, ajali ya vyombo vya usafiri wa majini, barabarani au kukanyaga umeme, Serikali hutoa kauli nzito na kuahidi kumchukulia hatua kali mtu yeyote atakayebainika kuhusika kuonyesha kuwa haitavumilia uzembe wa aina yoyote lakini baada ya muda, hali hubaki ileile bila ufuatiliaji.

Nani alaumiwe?

Mkurugenzi mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra), Ahmed Kilima anasema ajali za barabarani zinasababishwa na mazingira makubwa matatu ambayo ni makosa ya kibinadamu, ubovu wa miundombinu na ubovu wa magari.

Kilima anataja makosa ya kibinadamu kuwa ni mazingira ya uzembe wa dereva, ulevi, utoaji wa leseni kwa madereva wasiokuwa na ujuzi wa kutosha, ukaguzi mdogo wa mabasi na malori yanayosafiri mikoani, abiria kushabikia mwendo kasi na udhaifu wa wamiliki wa mabasi na malori kuajiri madereva wasio na uwezo.

“Kwa hiyo, siwezi kusema nani alaumiwe lakini mazingira yanaonyesha madereva na wamiliki wanahusika zaidi kwa upande wao kabla ya kuangalia makosa mengine yanayotokana na mamlaka husika,” alisema Kilima.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua), Godwin Ntongeji anasema ili kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la ajali nchini, ni lazima ukaguzi wa mabasi na madereva ufanyike mara kwa mara.

“Hakuna ukaguzi na watu wanaendelea kufa njiani, ajali nyingine siyo makosa ya dereva ila ni ubovu wa mabasi yenyewe. Jeshi la Polisi lina wajibu wa kukagua kuanzia leseni za madereva mpaka uchakavu wa mabasi, hivyo, haliwezi kukwepa lawama kwa namna yoyote juu ya vifo vya Watanzania,” anasema.

Msemaji wa Sumatra, David Mziray anasema jukumu la mamlaka hiyo ni kutoa leseni za biashara tu kwa wamiliki wa mabasi na malori na kwamba hakuna basi au lori linalokabidhiwa leseni bila kuwa na utambulisho wa dereva mwenye sifa zote.

“Sisi hatuwezi kuhoji ubora wa magari au dereva kwa sababu anakuwa amekuja na vyeti vinavyoonyesha amethibitishwa na Jeshi la Polisi kwamba ana sifa zote, kwa hiyo, tunatoa leseni kwa ajili ya biashara ya kubeba abiria au mizigo,” anasema Mziray.

Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Malori Tanzania, Clement Masanja anasema Serikali imeshindwa kusikiliza vyanzo vya ndani vya ajali hizo kutoka kwa madereva wa malori. Anasema kuwa jumla ya mabasi yanayotoka na kuingia kila siku katika Kituo cha Mabasi Ubungo ni wastani wa 300 huku takriban asilimia 50 yakiwa mabovu.

Masanja anasema lazima Serikali ikubali kuhusika na ajali za barabarani kutokana na ubovu wa miundombinu na kushindwa kufanya ukaguzi wa mabasi mabovu. Kuna wakati Serikali iliwataka wamiliki wa mabasi kufunga vidhibiti mwendo lakini viliondolewa na kuna wakati Jeshi la Polisi lilipewa kamera kwa ajili ya kupima mwendo kasi, lakini havitumiki ipasavyo.

Mnadhimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Johanes Kahatano anasema licha ya madereva kupinga, msimamo wa Serikali utabakia kuwa mwendokasi wa kilomita 80 kwa saa.

“Pamoja na changamoto ya miundombinu ,lakini kupunguza mwendokasi kutasaidia sana, hatuwezi kuendelea kuona ajali zikitokea kwa mazingira ya mwendokasi,” anasema.

Kuhusu ukaguzi wa mabasi na leseni za madereva, Kahatano anakiri kuwa ni changamoto kwa Serikali kutokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa kwani wamekuwa wakikagua mabasi hayo kwa macho tu bila kujihakikishia undani wa basi kama ni bovu au la. “Lakini kwa ukaguzi wa leseni tunajitahidi sasa kwani hatuwezi kuitoa leseni mpaka dereva afanyiwe majaribio. Kuhusu mazingira ya rushwa katika leseni siwezi kuwa na ushahidi kwa sababu hatujashuhudia tukio la rushwa katika utoaji wa leseni,” alisema Kahatano.

Majanga

Mei 21, 1996 ilitokea ajali mbaya ya kuzama meli ya mv Bukoba usiku ikiwa abiria kati ya 750 na 800 pamoja na wafanyakazi 37.Kati ya hao, 114 waliokolewa, maiti 391 ziliopolewa na kuzikwa katika makaburi ya Igoma, nje kidogo ya Jiji la Mwanza. Miili mingine ilichukuliwa na jamaa kuzikwa kwao. Miili 332 haikupatikana.

Serikali ilifungua kesi dhidi ya aliyekuwa nahodha wa mv Bukoba, Jumanne Rume-Mwiru (sasa marehemu); Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari, Gilbert Mokiwa; aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Bukoba, Alphonce Sambo na aliyekuwa Maneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila. Kesi hiyo Na. 22 ya 1998, ilianza kusikilizwa Mei 14, 2001.

Wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo iligundulika kwamba meli hiyo iliyojengwa na kampuni ya Kibelgiji, siku ya uzinduzi Julai 27, 1979 ilibainika haikuwa thabiti na ilikosa uwiano. Hukumu ya kesi ilitolewa Novemba 29, 2002 na washitakiwa wote walishinda. Serikali iliahidi kukata rufaa, lakini hadi leo haijafanya hivyo.

Mwaka 1998, basi la No Challenge la mkoani Tanga lilipata ajali iliyosababisha vifo vya abiria wapatao 70 kutokana na kile aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Simon Sirro kudai ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa basi hilo. Baadaye basi hilo lilibadilishwa jina na kuitwa Tashrif lakini nalo lilisababisha vifo vya watu 27 katika ajali iliyotokea Korogwe.

Halafu ukaja mfululizo wa matukio ya mabasi kugongana na treni pia magari moshi hayo kugongana yenyewe. Kwa mfano, Juni 24, 2002 ilitokea ajali mbaya ya treni kuwahi kutokea barani Afrika mkoani Dodoma. Treni iliyobeba abiria 1,200 ilirudi kinyumenyume katika kilima kidogo na kugongana na treni ndogo ya mizigo na kusababisha vifo vya watu 281. Ajali hiyo ilisababishwa na kushindwa kwa breki za treni hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam, lakini hakuna aliyewajibishwa.

Machi 11, mwaka huu ilitokea ajali mbaya ya barabarani katika Kijiji cha Changarawe wilayani Mufindi katika Mkoa wa Iringa baada ya basi la Majinjah lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam kugongana na lori la mizigo. Watu 50 walikufa na wengine 37 kujeruhiwa. Sababu za ajali hiyo imeelezwa kwamba nikuwapo kwa shimo la muda mrefu katika eneo hilo la barabara.