Ujerumani kupitisha sheria ya kujitolea viungo vya mwili

Waziri wa Afya wa Ujerumani, Jens Spahn

Muktasari:

Chini ya mpango huo, watu watatakiwa kueleza mapema kama wako tayari viungo vyao vya mwili kuondolewa baada ya kufa kwa ajili ya kutumika kuwawekea wagonjwa wenye mahitaji

Berlin, Ujerumani. Waziri wa Afya wa Ujerumani, Jens Spahn ameweka msukumo katika harakati za upatikanaji wa viungo vya mwili kwa ajili ya kuwawekea wagonjwa wanaovihitaji, akitaka kila mtu kuwa na uwezekano wa kujitolea viungo vyake baada ya kufa isipokuwa tu kwa wale watakaopinga mpango huo.
Lengo la sheria hiyo ya kutangaza mapema kuwa tayari kujitolea kiungo cha mwili kama vile figo, ni kukabiliana na ongezeko la wahitaji ambalo sasa limefikia watu 10,000, huku vifo vya watu wanaokufa, wakati wakisubiri kubadilishiwa viungo hivyo kufikia watu 2,000 kwa mwaka.
Chini ya mapendekeo hayo mapya, wananchi watatakiwa kueleza kama wanapinga mpango wa kujitolea viungo vyao au tishu zao kuvunwa baada ya kufikia hali ya ugonjwa ambayo kiuhalisia ni kama wameshakufa.
Wale ambao watajibu "hapana", majina yao yataingizwa katika orodha ya msajili wa taifa inayoratibiwa na wizara ya afya, wakati wengine watachukuliwa kama wahisani wa kujitolea viungo vyao, kanuni ambayo iko karibu katika nchi nyingi barani Ulaya.
Suala hili litamaanisha kubadilisha sheria ya sasa ya Ujerumani, ambayo inataka watu waeleze kama watakuwa tayari kwa hiari yao kujitolea viungo vyao.
Ndugu wa karibu watakuwa na uwezo wa kuzuia viungo hivyo kuchukuliwa kama wataweza kutoa hoja zinazoshawishi kuwa ndugu yao angeweza kupinga mpango huo.
Waziri wa Afya, Spahn kutoka chama cha CDU alisema kuna karibu takriban wagonjwa 10,000 wanaosubiri kuwekewa viungo vya mwili kutoka kwa watu wengine na kwamba mwaka 2017 kulikuwa na watu 800 waliojitolea viungo vyao, idadi ambayo ni ndogo kulinganisha na miaka mingine.
"Kila mmoja wetu anaweza kuwa anahitaji kuwekewa kiungo kesho," alisema Spahn katika mkutano na waandishi wa habari jijini Berlin, alipowasilisha mpango huo akiwa na wabunge wa vyama vya kifahidhina vya CSU, Social Democrats (SPD) na Die Linke.
Spahn alisema idadi ya watu wanaoweza kutoa viungo vyao nchini Ujerumani ni kubwa kutokana na utafiti kuonyesha kuwa asilimia 80 ya watu waliojibu swali kuhusu suala hilo walikubaliana nalo.
Chini ya taratibu za sasa, watu wanaweza kusaini kadi inayoonyesha yuko tayari kutoa kiungo na kuiweka katika mfuko wake ili kama wakifa, hospitali zinajua kuwa zinaweza kuchukua viungo vyao. Ni asilimia 30 tu ya Wajerumani wenye kadi hizo.
"Idadi ni mara kumi zaidi ya watu wanaosubiri kuwekewa viungo kulinganisha na idadi ya viungo vinavyowekwa kwa watu kila mwaka," alisema mbunge wa SPD, Karl Lauterbach.
"Kila mwaka, takriban watu 2,000 walio katika orodha ya kusubiri kuwekewa viungo, hufariki."
Baadhi ya wabunge wamepinga hatua hiyo.
Mbunge wa CSU, Stephan Pilsinger aliubatiza mpango huo wa Spahn "ni tata kimaadili" na kwamba unawafanya wagonjwa wawe kama "ghala la spea". AFP