VIDEO: Ujerumani yaikabidhi JWTZ hospitali ya kisasa

Muktasari:

  • Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limekabidhiwa hospitali ya kisasa yenye thamani ya Sh5.6 bilioni iliyojengwa na Serikali ya Ujerumani

Monduli. Serikali ya Ujerumani jana Jumatatu Mei 6, 2019 imekabidhi majengo na vifaa vya hospitali ya kisasa ya Kanda ya  Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyojengwa wilayani Monduli mkoa wa Arusha.

Hospitali hiyo imegharimu cha Sh5.6 bilioni.

Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Dk Detlef Waechter  amemkabidhi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Hussein Mwinyi funguo za hospitali hiyo katika hafla iliyofanyika wilayani Monduli jirani na Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA).

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Mwinyi amesema hospitali hiyo itakuwa na manufaa makubwa sio kwa jeshi tu bali hata kwa jamii ya Monduli na mkoa wa  Arusha.

"Katika hospitali hii ambayo itatoa huduma zote ikiwamo upasuaji, tunatarajia kutolewa huduma kwa wanajeshi na wananchi wa kawaida na takwimu zinaonyesha asilimia 80 ya wananchi ndio watanufaika huku wanajeshi wakiwa ni asilimia 20," amesema

Amesema hospitali hiyo inatarajiwa kupunguza gharama za matibabu ya maofisa wa jeshi na wanajeshi katika hospitali binafsi na nje ya nchi.

"Kwa niaba ya Serikali tunaishukuru sana Serikali ya Ujerumani kwa kusaidia ujenzi wa hospitali hii ambayo ni sehemu tu ya misaada mingi ambayo imekuwa ikitoa ikiwamo ujenzi wa chuo cha jeshi na kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya," amesema.

Pia, hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuboresha huduma za afya nchini na tayari vituo kadhaa vya afya na hospitali zimejengwa maeneo mbalimbali nchini.

Naye Balozi Waechter ameema Serikali ya Ujerumani, itaendelea kuisaidia miradi mbalimbali nchini Tanzania.

Awali, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo amesema ujenzi wa hospitali hiyo na vifaa vyake ni sehemu tu ya miradi ambayo imekuwa ikifadhiliwa na Ujerumani.

Jenerali Mabeyo amesema Ujerumani pia imetekeleza miradi mbalimbali katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya.

"Ujerumani imesaidia pia ujenzi wa chuo cha tiba cha Jeshi ambacho sasa kimeaza kutoa wahitimu wenye shahada," amesema.

Jenerali Mabeyo amesema hospitali hiyo sasa itakuwa ni ya Kanda ya JWTZ na itatoa huduma bora kama zilivyo hospitali za rufaa.

Mkuu wa tiba jeshini, Meja Jenerali  Denis Janga amesema hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 300 kwa siku na kulaza watu 50 wakati mmoja.

Meja Jenerali Janga alisema huduma zote za upasuaji zikiwamo za uzazi, zitatolewa sambamba na huduma nyingine muhimu kama meno na nyingine.

"Hii ni moja ya hospitali za kisasa na tutaleta hapa wataalamu wa kutosha ili kuweza kutolewa huduma bora za afya kwa wanajeshi na wananchi wa kawaida," amesema.