Ujumbe wa Majaliwa kwa mtandao wa maendeleo wa Aga Khan

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), kukamilisha majadiliano yao na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili watumiaji wa bima za NHIF waweze kutibiwa katika hospitali

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), kukamilisha majadiliano yao na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili watumiaji wa bima za NHIF waweze kutibiwa katika hospitali zake.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Mei 28,2019 wakati Majaliwa alipokutana na viongozi kadhaa wa AKDN na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ofisini kwake bungeni Jijini Dodoma.

 Majaliwa amesema Serikali inatambua mchango unaotolewa na taasisi ya AKDN katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya hapa nchini.

 “Nilijionea kazi kubwa inayofanyika pale Hospitali ya Aga Khan, Machi, mwaka huu, niliongea na wagonjwa na kupata maoni yao, lakini kikubwa tu mpunguze gharama na muimarishe huduma zenu,” amesema.

Amewapongeza viongozi hao kwa utoaji wao wa huduma kwenye sekta nyingine kama elimu, maji na kilimo. “Tunategemea mtaendelea kuimarisha huduma hizo ili ziwasaidie Watanzania wengi zaidi,” alisisitiza.

Aidha, viongozi hao walikutana na Waziri Mkuu ili kumuarifu juu ya mpango wa taasisi hiyo wa kuanzisha kituo maalumu cha matibabu ya saratani nchini (Specialised Cancer Care Facility) ambao unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 15 9 (zaidi ya Sh34bilioni).

 Kituo hicho kitaendeshwa kwa ubia baina ya hospitali za Ocean Road, Muhimbili, Bugando na Aga Khan.

 Awali, akitoa maelezo kuhusu mpango wa kujenga kituo hicho, Mwakilishi Mkazi wa AKDN, Amin Kurji alisema wameshawasiliana na hospitali zote tajwa na sasa wanashirikiana na wataalamu wa Wizara ya afya ili kukamilisha suala hilo. 

“Tatizo la saratani hapa nchini ni kubwa kwa sasa. Lakini tunataka watu watambue kwamba ukiugua saratani haimaanishi kwamba ni adhabu ya kifo (it’s not a death sentence). Inaweza kutibika endapo mgonjwa atawahi kupata matibabu,” alisema Kurji.

Amesema kwa sasa hapa nchini hakuna kituo maalum cha matibabu ya saratani nchini lakini kitu cha pekee kuhusu kituo hicho ni uwepo wa huduma zinazotembea za upimaji na utoaji tiba hadi mikoani.

“Huduma hizi zitakuwa zinatolewa kwenye mikoa yote kupitia njia ya mtandao, ilhali vituo vikuu vya Dar es Salaam na Mwanza vitakuwa vikitoa majibu kwa madaktari husika,” alisema.

Amesema lengo ni kutoa elimu juu ya kuzuia, upimaji wa mapema na upatikanaji wa tiba (prevention, early diagnosis and cure).