Ujumbe wa Rais Magufuli kwa nchi za SADC

Monday August 5 2019

Rais John Magufuli akizungumza alipokuwa

Rais John Magufuli akizungumza alipokuwa akifungua maonyesho ya nne ya bidhaa katika wiki ya viwanda kwa nchi 16 wanachama wa SADC, kwenye Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam leo. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC) kufanya biashara kwa pamoja badala ya kufikiria kununua bidhaa nje lengo likiwa kukuza na kuimarisha sekta ya viwanda.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 5, 2019 wakati akizindua maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda kwa nchi 16 wanachama wa SADC, Dar es Salaam nchini Tanzania.

Amesema nchi za SADC zinapaswa kuweka kipaumbele kwenye teknolojia ya viwanda ndani ya nchi zao kabla ya kwenda mbali sanjari na hiyo pia zitumie malighafi kutoka katika nchi zao.

"Tununue malighafi ndani ya SADC, pia tunao vijana wengi wenye uwezo wa sayansi na teknolojia wengi wanakwenda kununua teknolojia kwa gharama kubwa ilhali kuna vijana wenye vipaji ndani ya nchi hizi 16.”

"Viwanda vidogo ndivyo hukua na kuwa vikubwa kukiwa na mazingira wezeshi kukuza uchumi na viwanda, nishati ya umeme wa uhakika, usafiri tutafika tunapopatarajia," amesema.

Rais Magufuli pia amezitaka nchi hizo kushughulikie vikwazo vyote vinavyojitokeza ikiwemo tozo mbalimbali na vikwazo vya mipakani ili kuwezesha viwanda na biashara.

Advertisement

Advertisement