Unapopita kwenye majaribu usinung’unike wala kukata tamaa, upo mpango wa Mungu

Sunday February 10 2019Nabii Elisha Muliri

Nabii Elisha Muliri 

By Nabii Elisha Muliri

Shaloom, shalom watu wa Mungu. Jina langu naitwa Nabii Elisha Muliri kutoka kanisa la Ebenezer, Kinondoji Studio jijini Dar es Salaam. Somo letu Jumapili ya leo linatoka katika kitabu cha Mwanzo sura ya 16 kuanzia mstari wa saba. Somo hili linaongea kuwa ‘Maji yako yatatokea’.

Biblia inasema hivi ‘ Baadaye malaika wa Bwana akamkuta kwenye chemchemi ya maji nyikani, kwenye chemchemi iliyo njiani kuelekea Shuri.

Naye akaanza kusema: “Hagar, mjakazi wa Sarai, umetoka wapi nawe unaenda wapi?” Naye akajibu: “Mimi ninakimbia kutoka kwa Sarai bimkubwa wangu.” Na malaika wa Yehova akaendelea kumwambia: “Rudi kwa bimkubwa wako ujinyenyekeze chini ya mkono wake.”

Ndipo malaika wa Bwana akamwambia: “Nitauzidisha sana uzao wako, hivi kwamba hautahesabiwa kwa sababu ya wingi wake.”

Tena, malaika wa Yehova akamwambia: “Tazama una mimba, nawe utazaa mwana, nawe utamwita jina lake Ishmaeli; kwa kuwa Yehova ameyasikia mateso yako.

Na yeye atakuwa kama pundamilia. Mkono wake utamwinukia kila mtu, na mkono wa kila mtu utamwinukia yeye, naye atakaa mbele ya uso wa ndugu zake wote.”

Biblia inaandika kwamba Hagar alikuwa msichana ambaye ni mfanyakazi wa nyumba ya Ibrahim, lakini Sarai mke wa Ibrahim alikuwa hazai.

Ibrahim akataka kuwa na mtoto lakini Sarai akamwambia Ibrahim kwa sababu wewe unahitaji mtoto ingia kwa mjakazi wangu Hagari ukazae mtoto.

Ibrahim akazaa mtoto na Hagar. Mtoto alipokuwa mambo yakaanza kuharibika na mtoto huyo akawa sababu ya chuki ndani ya kaya ya Ibrahim.

Sasa Biblia inasema kwamba Sarai akakasirika na kumwambia Ibrahim mtoe binti huyu hapa maana amenidharau.

Ibrahim akamlilia Mungu na Mungu akamwambia fanya lile ambalo Sarai ameomba. Kumbe ulikuwa uasi na huo uasi mbaya mpango wa Mungu ulikuwepo.

Kuna mambo mengi yamekutokea kwenye maisha yako nawe unadhani Mungu amekuacha ndani ya hayo mambo magumu, mpango wa Mungu upo.

Unaweza kufukuzwa ndani ya nyumba na kutolewa nje kama mbwa ukaambiwa usirudi na kama ukirudi nitakuingiza kisu ukaumia sana na kulia ukisema ‘jamani wamenikataa, nitaenda kwa nani? Nitaishije? Usiogope kwa sababu Mungu anakuepusha na mabaya ambayo yangeweza kutokea, hivyo ni mapenzi ya Mungu.

Hata kama yatakutokea mengi magumu usiogope kwa sababu Mungu atakuponya nayo yote. Acha kulia na kunung’unika kwa sababu ya hayo unayopitia, mambo mengi unapitia kwa sababu wewe unayo hatma kubwa.

Anayejaribiwa sana, huinuliwa sana anayepigana sana hupata ushindi mkubwa sana, anayekimbia sana kuliko wengine huwa anaenda mbali zaidi kuliko wenzake.

Biblia inaeleza kuwa Hagar alipofika jangwani mtoto alianza kulia. Inasema wakati mtoto alipoanza kulia jangwani.

Kumbuka ukilia jangwani hakuna mtu wa kukusikia, ni bora ulie nyumbani kwa sababu wapo majirani na ndugu wanaweza kukusikia wakakusaidia.

Bora ulie barabarani kwa sababu watu watakuona na kukusaidia. Hata ukilia shambani mwenye shamba la jirani atakusikia lakini jangwani huko hakuna wa kukusikia.

Ni kweli wakati mwingine unaweza kulia sana kwa ugonjwa ukajiona upo peke yako kwa sababu madaktari wameshindwa kukusaidia.Unavyo vidonge na dawa nyingi lakini vyote havikusaidii.

Kuna wakati unaweza jikuta unalia na kila kitu chako kinalia kiasi cha kukata tamaa na hata kutamani kujiua, Biblia inasema usife moyo wala kukata tamaa kwa sababu katika hayo yote, upo mpango wa Mungu juu yako.

Kumbuka Mungu hawezi kukuacha hata siku moja anatembea kwenye ahadi zake cha msingi usikate tamaa, endelea kumuita wakati wote. Dhahabu haiwezi kuwa dhahabu mpaka ipite kwenye moto mkali.

Usife moyo, mlilie Mungu yeye atakusaidia, maana katika hayo magumu unayopitia kwenye maisha upo mpango wake wa kutaka kukuvusha.

Hata kama machozi yako yamekuwa ya Jangwani wala usisahau kuwa katika jangwa, upo mpango wa Mungu na Mungu atakusaidia. Inua mikono yako juu mbele za Mungu ukimshukuru na sema ‘Halleluya’ kwa sababu yeye ndiye Mungu mkuu anayejua kesho yako.

Jambo pekee na la muhimu usiache ibada, usiache kukaa karibu na Mungu endelea kulitaja jina la Yesu katika maisha yako.

Mungu akubariki sana na ninakutakia Jumapili njema yenye mafanikio tele. Karibu kanisani.

Amen.

Imeandaliwa na Tumaini Msowoya

Advertisement