Unep yazitaka Serikali kushirikisha wadau kuokoa mazingira

Picha na mtandao

Muktasari:

 

  • Hamasa hiyo imetolewa na wajumbe mbalimbali walioshiriki mkutano wa nne wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA), wakiongozwa na Rais wa mkutano huo Siim Kiisler alipokuwa anafanya majumuisho

Nairobi, Kenya. Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) umesema juhudi za kupambana na uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko ya tabianchi ziendelezwe kwa kuwahusisha wadau wengi zaidi.

Hamasa hiyo imetolewa  na Rais wa mkutano wa nne wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA), Siim Kiisler alipokuwa anafanya majumuisho.

Kiisler alisema kumekuwa na mwitikio mkubwa kutoka serikalini, asasi za kiraia hata kampuni na taasisi zilizo tayari kushiriki kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza.

"Takriban wajumbe 5,000 wamehudhuria, kujadili na kuridhia mapendekezo yaliyowasilishwa. Kukamilika kwa mkutano huu ni maandalizi ya ujao utakaojikita kuhakikisha kunakuwa na sheria za kusimamia maazimio yanayoridhiwa," alisema Kiisler.

Kwenye mkutano wa kwanza uliofanyika mwaka 2014, kulikuwa na wajumbe 1,500 tu waliohudhuria lakini kadri siku zinavyoenda ari inaongezeka zaidi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP na Katibu wa UNEA, Joyce Msuya amesema mkutano huo  umedhihirisha utayari wa wadau mbalimbali kushiriki kuyaokoa mazingira na kinachotakiwa ni kila  Serikali kuweka mikakati shirikishi.

"Nia ipo, tunachotakiwa ni kuongeza kasi ya mapambano. Asasi za kiraia zipo tayari kushirikiana na Serikali kupigana vita hivi," alisema Joyce.

Pamoja na mafanikio ya mkutano huo, Joyce alisema kulikuwa na changamoto za hapa na pale ambazo, hata hivyo, hazikuathiri mchakato mzima.

"Chakula cha kukidhi mahitaji ya watu wenye utamaduni tofauti lilitupa tabu kidogo lakini hakuna kilichoharibika," alisema.

Joyce aliitumia nafasi hiyo pia kutoa pole kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao kwenye ajali ya ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia. Umoja wa Mataifa umepoteza wafanyakazi 22 katika ajali hiyo.

Kwa maandalizi ya mkutano ujao, sekretarieti ya UNEP inayoundwa na mawaziri wa mazingira imemchagua waziri wa hali ya hewa na mazingira kwa Norway, Ola Elvestuan kuwa Rais wa mkutano ujao.