Upelelezi kesi ya Wambura bado

Muktasari:

Upande wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, kuwa wanapitia nyaraka muhimu kabla ya kukamilisha upelelezi.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa wanapitia nyaraka muhimu kabla ya kukamilisha upelelezi.

Wambura anakabiliwa na mashtaka 17 yakiwamo ya kutakatisha zaidi ya Sh100 milioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2019.

Wakili wa Serikali, Batilda Mushi, ameieleza mahakama hiyo  leo April 11, 2019 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Mushi, amedai mbele ya Hakimu Kelvin Mhina, kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kwa sasa wanapitia nyaraka muhimu ambazo hawawezi kuziweka wazi.

"Upelelezi wa shauri hili haujakamilika na upande wa mashtaka  tunaendelea kupitia nyaraka muhimu, hatuwezi kuzisema ni  zipi ila upande wa utetezi wajue tu kwamba kuna nyaraka muhimu tunazifanyia kazi kabla ya kukamilisha upelelezi wa kesi hii," amedai Mushi.

Mushi baada ya kueleza hayo, wakili wa mshtakiwa, Majura Magafu, aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo isonge mbele.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi April 25, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana.

Kwa mara ya kwanza, Wambura alifikishwa Kisutu Februari 11, 2019 akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwamo ya kutakatisha  zaidi ya Sh100 milioni.

Katika mashtaka hayo 17; shtaka moja ni la kughushi; shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004 sehemu isiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Siku hiyo, Wambura kwa nia ya kutapeli alitengeneza barua ya  kughushi ambayo haina kumbukumbu namba akionyesha imeandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa  kampuni ya Jeck System, akidai kurejeshewa malipo ya mkopo wa Dola 30,000 za Marekani na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka la kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, mshtakiwa alitoa barua iliyokuwa haina kumbukumbu namba ya Julai 6, 2004, akijifanya kuwa iliandikwa na E. Maganga  akionyesha kuwa anadai mkopo wa Dola 30,000 za Marekani  na riba walioikopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, kuanzia  shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia zaidi Sh95 milioni kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa ni sehemu ya malipo ya jumla ya fedha mbalimbali na riba kutoka kwa kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa siyo kweli.

Pia, katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 17, 2015 katika ofisi za TFF,  kwa njia ya udanganyifu mshtakiwa alijipayia Sh10 milioni kutoka TFF kwa kuonyesha kuwa ni malipo ya Dola 30,000 za Marekani na riba kutoka kwenye kampuni ya Jeck, jambo ambalo siyo kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadaiwa kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014 makao makuu ya shirikisho hilo alijipatia Sh25 milioni kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia, shtaka jingine la utakatishaji fedha haramu, mshtakiwa anadaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21, 2015 alijipatia Sh75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali na zimetokana na shtaka la kughushi.