Upungufu wa madawati walazimu watoto kwenda na vigoda shuleni

Sunday February 10 2019

 

By Ngollo John, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Elimu ya bila malipo kuanzia shule za awali hadi sekondari imeendelea kukabiliwa na changamoto za miundombinu, ikiwamo madarasa na vifaa vya kujifunzia kutokana na wingi wa wanafunzi.

Wakati kukiwa na uhaba wa vyumba vya madarasa katika baadhi ya shule, madawati pia ni tatizo katika shule nyingi.

Kutokana na upungufu wa madawati katika shule mbalimbali, baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi Mkolani na Ibanda jijini Mwanza wameamua kwenda na mifuko ya nailoni au vigoda shuleni kwa ajili ya kukalia.

Shule hizo pia zinatumia maturubai kuwatandikia chini ili wanafunzi wa darasa la kwanza waweze kukalia.

Akizungumza na Mwananchi, mwanafunzi wa shule ya msingi Mkolani, Neema Marco alisema analazimika kwenda na mfuko wa kukalia kwa sababu madawati hayatoshelezi,

“Tunajifunza kwa tabu, darasani tunakaa zaidi ya wanafunzi 100, madawati yaliyopo ni machache hivyo wengine tunalazimika kwenda na mifuko ili tukalie tusichafuke.”alisema.

Mkazi wa mtaa wa Ibanda, Sostenes Malungu alisema uhaba wa madawati umewalazimu wazazi na wale kuwatengenezea watoto wao mifuko au vigonda vya kwenda kukalia.

Iren Joseph anayesoma darasa la kwanza katika shule hiyo aliiomba Serikali kushirikiana na wazazi kutatua changamoto hiyo kwani wanashindwa kujifunza kuumba herufi vizuri.

Akizungumzia utatuzi wa changamoto hiyo, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba alisema wametenga Sh120 milioni kutengenezea madawati.

Alisema tayari fedha hizo zimeanza kusambazwa kwenye kila shule na kwamba zaidi ya madawati 54,000 yanahitajika ili kukidhi idadi ya vyumba vya madarasa 1,800 ambavyo vinahitajika kujengwa katika jiji hilo lenye shule 80.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ibada, Neldomina Nyirenda alisema kutokana na upungufu huo wanalazimika kuwagawa wanafunzi kusoma katika mikondo miwili.

“Wanafunzi wengine wanaingia darasani saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana huku wengine wakiingia saa sita hadi saa 10 jioni,” alisema Nyirenda.

Advertisement