VIDEO: Rugemalira awaweka benchi mawakili, asimama kujitetea mwenyewe

Thursday June 20 2019

Mshtakiwa wa kesi ya uhujumu uchumi, James Rugemalira ,Mahakama ya Rufani

 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mshtakiwa wa kesi ya uhujumu uchumi, James Rugemalira jana alizira kuendelea na usikilizwaji wa rufaa yake na kuamua kuachana nayo, baada ya Mahakama kumkatalia kutoa hoja ambazo zilikuwa hazihusiani na rufaa yake iliyoko mahakamani kabla ya kuombwa na kukubali kubadili uamuzi wake huo.

Mfanyabiashara huyo maarufu ambaye amekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka miwili sasa akikabiliwa na mashtaka 12, alitoa kali hiyo jana katika Mahakama ya Rufani ilipokaa kusikiliza rufaa yake alipoamua kujitetea mwenyewe akiwaweka kando mawakili wake.

Katika rufaa hiyo, Rugemalira anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kumnyima dhamana, uliotolewa na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo Firmin Matogolo, Agosti 30, 2019.

Aliamua kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo baada ya wakili wake, Pascal Karama kumtuliza na kumshawishi kuitumia fursa hiyo kujaribu kwa mara nyingine kuishawishi Mahakama imwachie huru kwa dhamana wakati wakisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yao ya msingi.

Kabla ya kuzira kuendelea na rufaa hiyo, iliyosikilizwa na jopo la majaji watatu, Richard Mziray (kiongozi), Winfrida Korosso na Ignas Kitusi, kwanza Rugemalira licha ya kuwa na mawakili wawili, aliiomba Mahakama imruhusu atoe hoja zake yeye mwenyewe mawakili wake wakimsikiliza.


Advertisement

Advertisement