Vijana CUF wamfuata Maalim Seif ACT-Wazalendo

Muktasari:

  • Waliokuwa viongozi wa Jumuiya ya Baraza la  Vijana wa CUF (Juvicuf) wametangaza rasmi kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo kwa maelezo kuwa wanataka kuunganisha nguvu na kuimarisha upinzani kwa maendeleo ya Tanzania

Dar es Salaam. Waliokuwa viongozi wa Jumuiya ya Baraza la Vijana wa CUF (Juvicuf) wametangaza rasmi kujiunga na chama ACT-Wazalendo kwa maelezo kuwa wanataka kuunganisha nguvu na kuimarisha upinzani kwa maendeleo ya Tanzania.

Viongozi hao wakiongozwa na aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Juvicuf,  Aisha Said  leo wamekabidhiwa kadi za ACT-Wazalendo katika ofisi za chama hicho, Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Wengine waliombatana na Aisha ni aliyekuwa mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa jumuiya hiyo, Anderson Ndambo na mkurugenzi wa habari na mawasiliano kwa umma, Abeid Khamis Bakari.

Kabla ya kukabidhiwa kadi, Bakari amewaambia wanahabari kuwa wamekwenda na kadi zaidi ya 1,000 za vijana wa CUF ambao wapo tayari kujiunga na ACT.

"Tunashukuru kwa kutupokea, tumekuja kwa ajili  na kuunganisha nguvu ndani ya upinzani ikiwamo kuimarisha ngome ya vijana wa ACT-Wazalendo," amesema Abeid.

Amesema uamuzi wa kuungana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye sasa ni mwanachama wa ACT si kufuata vyeo bali kutafuta jukwaa jingine litakalosaidia kutetea maslahi ya Taifa.

Kwa upande wake. Aisha amesema: “ Tumemfuata jemedari wetu, Maalim Seif asiyependa fujo. Pemba asilimia kubwa ya vijana wapo pamoja na ACT-Wazalendo baada ya yeye kuja chama hiki.”

Mwenyekiti wa ngome ya vijana ya ACT-Wazalendo, Bakari Likapo amesema ujio wa vijana hao na Maalim Seif ndani ya chama hicho umewapa faraja kubwa katika kuhakikisha upinzani unaimarika.

"Tanzania kuna vyama vingi lakini Maalim Seif ameamua kuja kwetu ni faraja ya kipekee kwa chama hiki. Tunamshukuru kwa kuja na kuendeleza mapambano.”

" Tupo pamoja  na uamuzi wao na tunawaambia ACT-Wazalendo ni sehemu salama watapata ushirikiano wote.

Hii inatoa picha kwenye jamii kuwa ACT ni chama chenye misingi imara,” amesema.