VIDEO: Viongozi 11 kitanzini ajali ya moto Morogoro

Wednesday August 14 2019

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar/Moro. Uamuzi wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuunda timu ya kuchunguza chanzo cha ajali ya moto iliyotokea mjini Morogoro siku tatu zilizopita, utawaweka hatarini viongozi 11.

Hali hiyo inatokana na watendaji hao kuwa na majukumu ya kusimamia ulinzi na usalama wa raia na mali zao sambamba na uokoaji, yanapotokea majanga, kama la moto uliotokana na ajali ya barabarani.

Haitashangaza viongozi hao ama walio chini yao wakahojiwa na timu hiyo inayotakiwa kukamilisha kazi yake Ijumaa wiki hii.

“Hii tume inaanza kazi leo (juzi), hadi Ijumaa (Agosti 16) inipe taarifa yake na hata kama mimi sijawajibika initaje,” alisema Majaliwa juzi wakati akizungumza na wananchi wa Morogoro kuhusu ajali hiyo.

“Ajali ya namna hii si mara ya kwanza, ilitokea Mbeya eneo la Mbalizi.”

Majaliwa alisema ni lazima kujua kama ajali, ambayo hadi jana ilikuwa imeua watu 75, kila mmoja alitimiza wajibu wake.

Advertisement

Alihoji kitendo cha wananchi kujichotea mafuta na kuchomoa betri ya lori hilo bila kuzuiwa licha ya kuwa eneo hilo kuwa karibu na kituo cha polisi cha Msamvu.

Kwa mujibu wa majukumu yao, viongozi wanaoweza kuwekwa kiti moto ni pamoja na Kangi Lugola, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Simon Sirro (Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP), Dk Stephen Kebwe (mkuu wa mkoa), Regina Chonjo (mkuu wa wilaya ya Morogoro) na Michael Deleli (mkuu wa kikosi cha trafiki Morogoro).

Wengine ni Gilbert Mvungi (mkuu wa Zimamoto mkoa), Wilbroad Mutafungwa (kamanda wa polisi Morogoro), Thobias Andengenye (mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji), Fortunatus Muslimu (mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani) na Ahimidiwe Msangi (mkuu wa kituo cha polisi Msamvu) na Masala Mugema (mkuu wa trafiki kituo cha polisi Msamvu) na askari polisi waliokuwa katika doria siku ajali hiyo.

Ajali hiyo ilitokea Mtaa wa Itigi, Msamvu, mita 200 kabla ya kufika kituo kikuu cha mabasi cha Msamvu, baada ya lori la mafuta kupinduka na baadaye kushika moto uliotokana na ama cheche kutoka kwenye betri la lori ama mtu aliyekuwa akivuta sigara ama majiko ya mamalishe waliokuwa jirani.

Picha za video zinaonyesha lori hilo likiwa limepinduka barabarani na mafuta yakichuruzika kuelekea kando mwa barabara. Watu waliokuwa na madumu ya ujazo mbalimbali wanaonekana wakichota mafuta hayo kabla ya moto kuwaka.

Tukio kama hilo limewahi kutokea mkoani Mbeya ambako lori la mafuta lilipinduka eneo la Kijiji cha Idwele wilayani Rungwe na wananchi kumiminika kuchota mafuta, lakini mmoja wao akaelekea kuchomoa betri la gari na makosa yake yalifanya cheche zitoke na mafuta kushika moto.

takriban watu 40 walipoteza maisha katika eneo hilo.

Katika siku za karibuni, baadhi ya viongozi wanawajibishwa au kuondolewa katika nafasi zao, na siku chache baadaye Rais John Magufuli hueleza sababu za uamuzi huo.

Na ajali za barabarani ni baadhi ya sababu zilizowafanya baadhi ya viongozi kuwajibishwa.

Baada ya kutengua uteuzi wa Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani mwaka 2018, Rais alitaja sababu 13 za kumuondoa.

Moja ya sababu hizo ilikuwa ni mfululizo wa ajali za barabarani bila hatua kuchukuliwa.

“Nimechoka kutuma rambirambi. Kila siku inatoka (ajali) hii, inakuja hii na kwa bahati mbaya ni mimi pekee ndiye ninayetuma rambirambi,” alisema Rais Magufuli.

Katika sakata la madini, Rais aliwataka wote waliohusika kuwajibika na wito wake ulitekelezwa na baadhi ya mawaziri.

Advertisement