Viongozi wawalilia wafanyakazi wa Azam

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akizungumza wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa wafanyakazi wa kamapuni hiyo waliofariki kwenye ajali.Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Viongozi mbalimbali waliofika katika ofisi za Azam Media, Tabata kuaga miili ya waliokuwa wafanyakazi watano wa kampuni hiyo waliofariki katika ajali Singida wametoa salamu za pole kutokanba na msiba huo.

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wametoa salamu za pole kutokana na vifo vya wafanyakazi watano wa Azam Media waliofariki dunia kwenye ajali mkoani Singida jana Jumatatu Julai 8, 2019.

Wafanyakazi hao ni miongoni mwa watu saba waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Shelui mkoani Singida baada ya gari aina ya Toyota Coaster walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori.

Viongozi hao wametoa salamu zao katika ibada ya kuaga miili ya wafanyakazi hao inayoendelea nje ya ofisi za kampuni hiyo Tabata TIOT, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema “Nawapa pole  familia yote ya Azam, marehemu kwa kuondokewa na nduu zao. Ni msiba mzito na pigo kubwa kwa chombo cha habari na taasisi moja kuondokewa na watu watano kwa mpigo.”

“Ni pengo kubwa kwa sababu utaalamu  pia umepotea, hata unaona kitengo cha uzalishaji cha Azam kilikuwa na ubora  mkubwa kwa sababu ya utaalamu huu ambao umeondoka lwa pamoja, tunawapa pole,” amesema Makamba.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amewataka wanahabari kufanya kazi kwa utaalam ili kuwaenzi wafanyakazi hao.

“Tunawapa pole familia, Azam Media na Watanzania wote, ni jambo linalouma sana lakini ni uamuzi wa Mungu inabidi tuukubali. Kilichobakia ni kuendelea kuwaombea na kuwaenzi,” amesema Profesa Lipumba.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema “Kwa kweli tumepokea kwa masikitiko makubwa  taarifa zote za msiba wa vijana wetu hawa wadogo sana.”

“Nchi  nzima imeingia kwenye majonzi, chama chetu tunaungana na familia za marehemu, wafanyakazi, na menejimenti ya Azam na Watanzania wenzetu kuomboleza na kuwaombea maisha mema na roho zao zikapumzishwe pema peponi.”

Akitoa salamu za Chama cha Mapinduzi (CCM), Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, , Humphrey Polepole amesema, “Kwa niaba ya uongozi wa chama tunatoa pole kwa tasnia nzima ya habari lakini kwa upekee kwa Azam Media kwa msiba huu mkubwa.”

“Tunashiriki misiba lakini pahala pamoja kupotelewa na wafanyakazi watano ni msiba mkubwa, hii ni ajali kwa kweli ni tukio ambalo limetugusa sana, wakuu wa chama walishtushwa na ajali iliyochukua vijana wetu. Chama kinatoa pole nyingi kwa wote walioguswa na msiba huu.”

Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC),  Dk Ayub Rioba amesema kila mtu anapaswa kuzingatia sheria za barabarani ili kuepuka ajali.