Vita ya mfanyabiashara, DC Sabaya bado mbichi

Muktasari:

Ugomvi wa mmiliki wa Hoteli ya Weruweru River Lodge, Cuthbert Swai na mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya bado haujatulia baada ya mfanyabiashara huyo kumtaka mtendaji huyo wa Serikali kujibu hoja za tuhuma za rushwa na si kuanzisha mambo mapya

Hai. Ugomvi wa mmiliki wa Hoteli ya Weruweru River Lodge, Cuthbert Swai na mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya bado haujatulia baada ya mfanyabiashara huyo kumtaka mtendaji huyo wa Serikali kujibu hoja za tuhuma za rushwa na si kuanzisha mambo mapya.

Swai alitoa kauli hiyo jana Alhamisi Julai 25, 2019 mjini Moshi alipozungumza na Mwananchi ikiwa ni siku moja tangu Sabaya alipomtuhumu mfanyabiashara huyo kudhulumu ardhi mwanamke alipoulizwa kuhusu tuhuma za kushinikiza malipo ya kodi ili mdaiwa atoe chochote.

Lakini mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema suala hilo tayari liko Takukuru na hivyo hatalizingumzia.

Kwa mara ya kwanza, tuhuma hizo ziliibuliwa na Swai mapema wiki hii katika mkutano kati ya wafanyabiashara na maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Swai alimtuhumu Sabaya kuwa alitaka apewe fedha katika matukio manne tofauti na kwamba jumla ya fedha alizokwishachukua hadi sasa zinafikia Sh10 milioni.

Hata hivyo, Sabaya alikanusha tuhuma hizo wakati akizungumza katika eneo la mgogoro baina ya Swai na mjane aitwaye Marry Kiriwa katika kijiji cha Kimashuku, akisema kiini cha tuhuma za Swai ni yeye kuingilia mgogoro huo.

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Ijumaa Julai 26, 2019.